Tunafeli wapi uhifadhi wa chakula?

Muktasari:

Ni tabia ya binadamu kumsifia mtenda mema baada ya kufa. Hii ni tabia mbaya.

Ni tabia ya binadamu kumsifia mtenda mema baada ya kufa. Hii ni tabia mbaya.

Sasa leo kwa niaba ya Watanzania wote, bila kupepesa macho naomba nimsifie Rais wa awamu ya nne. Si mwingine, ni Jakaya Mrisho Kikwete. Kwa nini?

Mwanasiasa huyu, mimi namwita kwa jina la ‘mwamba’ aliingia Ikulu akiwa na falsafa moja ngumu kama cheo chake cha kijeshi kilichopo mabegani mwake kilivyoongea enzi hizo akiwa mvaa magwanda.

Aliingia Ikulu kupambana aifute kabisa njaa Tanzania. Akasikika akisema: “Watanzania, Kilimo kwanza!” Ndio. Alifanikiwa sana.

Zogo limebaki kwenye kulanguana tu chakula maana bei hazishikiki, kwa sababu tumekubaliana tuwauzie pia majirani zetu wenye njaa, na hao ndio wanaowafanya wakulima wawe na tamaa ya kutajirika huku wanyonge wakitaabika.

Ila, ukitembelea masoko yetu utagundua kuwa nusu ya mbogamboga na matunda, vipo dampo vimeharibika! Vimeharibika kwa kukosa wanunuzi. Sio masokoni tu, hata machinjioni nenda utakuta nyama zinaharibika.

Hii unaweza ukasema ni kufuru lakini ukienda mbali zaidi, utagundua kuwa wakulima, wavuvi na wafugaji wetu, hawana uelewa wa namna ya kuhifadhi vyakula hivyo ili vitusaidie baadaye.

Kuna kitu kinaitwa kwa lugha ya Kiingereza ‘Cold Room’ ambayo kwa Kiswahili fasaha siijui tafsiri yake rasmi na sanifu. Ila ninachojua ni chumba kikubwa chenye ubaridi wa kutosha kutunza matunda, mboga, nyama na samaki kwa zaidi ya miezi sita bila kupoteza rangi, ladha na hata utamu wake pia.

Niende mbali zaidi, ‘cold room’ ina uwezo wa kuwahifadhi wafu bila tatizo lolote. Cha ajabu nchini Tanzania, ukitaka kuiona cold room kirahisi, nenda kwenye mahoteli ya kitalii, supermarkets na kwenye vyumba vya kuhifadhia wafu katika hospitali kubwa za Serikali tu.

Ajabu sana. Cold room zilitakiwa zijengwe katika kila shamba la matunda na mboga, machinjio ya wanyama, masoko yote, maduka ya nyama, maziwa na mayai.

Aidha, vyumba hivi vilitakiwa vifungwe katika malori yanayo safirisha bidhaa hizo kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Lakini pia, Cold rooms zilitakiwa zijengwe katika kila zahanati na hospitali ili kupunguza msongamano wa wafu katika hopitali chache zenye huduma ya kuhifadhi wafu.

Mimi binafsi ni jasusi wa kujitegemea (Private Investigator) na ni fundi wa kujenga hizi cold rooms. Nimeshajenga chache hapa Tanzania.

Hata hivyo, kinachonisukuma kuongea na Watanzania leo kuhusu vyumba hivi ni baada ya kufanya uchunguzi na kugundua kuwa havipo nchini kwa sababu ya uelewa tu.

Wakulima, wafugaji na wavuvi wanatakiwa wapewe somo kuhusu umuhimu wa kuwa na cold rooms ili tuokoe mazao yetu yasiharibike kwa kuwa tutaweza kuhifadhi vyakula katika kwa muda mrefu bila tatizo lolote.

Kwa uelewa wangu mdogo, nina imani falsafa ya kilimo kwanza itakuwa na faida kwetu sote kwa kuwa tutakula mboga, matunda na vitoweo bila kujali ni msimu gani.

Kujenga cold rooms kunahitaji uwekezaji mkubwa kidogo, hivyo walalahoi hatutaweza maana chumba cha mita tatu kwa tatu kinagharimu takribani Sh30 ujenzi wake. Ila faida yake ni kuwa ukijenga, umejenga na itatumika zaidi ya miaka 50 bila tatizo.

Hapa, rai yangu ni wakulima, wafugaji na wavuvi wenye mitaji mikubwa wazijenge hizi cold rooms ili sisi wenye mbavu za samaki tukodishwe kuhifadhi mazao yetu.

Ila, ipo namna ya kujenga zenye gharama nafuu lakini zinakuwa sio imara na bora katika viwango vya kimataifa. Kifupi huwa hazidumu, zinaweza zikasaidia kuhifadhi kwa takribani miaka kumi hivi. Najua kuwa wapo wenye akili za kuvukia barabara ambao huwa hawaangalii mazuri ya mtu. Wao huangalia mabaya tu ya mtu na kumteta.

Naomba niseme tu kuwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete naye ni binadamu hivyo tukimtafuta mabaya yake hatutayakosa. Kilichobaki tusifiane kwa mazuri tunayoyafanya.

Hivyo, naomba tumsifu huyu mzee kwa mema aliyotufanyia Watanzania kabla hajafa ili asikie, achekelee, aongeze siku zake za kuishi duniani.

Jamani tukamilishe falsafa ya kilimo kwanza kwa kujenga hizi cold rooms ili tuokoe vyakula vinavyoharibika kabla Mungu hajatuhukumu kwa kosa la kuchezea vyakula makusudi. Kilimo Kwanza!

Dk John Haule ni mdau wa lishe Anapatikana kwa simu; 0768 215 956/0673 722 823.