Tunashindwa wapi kudhibiti vifungashio?

Tunashindwa wapi kudhibiti vifungashio?

Muktasari:

  • Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), imeshatangaza kuwa jana ilikuwa mwisho wa matumizi ya vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango vya ubora.


Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), imeshatangaza kuwa jana ilikuwa mwisho wa matumizi ya vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango vya ubora.

Ikaongeza kuwa operesheni maalumu itaendeshwa nchi nzima kuanzia leo kubaini wazalishaji na wasambazaji wa vifungashio hivyo visivyo na ubora unaotambulika na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Hii si mara ya kwanza kwa Serikali kutangaza au kuendesha kampeni za kuzuia matumizi ya vifungashio hivi ambavyo kwa hakika ni hatari kwa afya za binadamu na hata mazingira.

Tangu awamu zilizopita za Serikali, marufuku ya vifungashio hivi imekuwa ikitolewa sambamba na elimu kwa umma kuhusu hatari ya matumizi yake, lakini kinachoshangaza utekelezaji wa marufuku hiyo huwa ni kwa muda mfupi.

Si tu baadhi ya wazalishaji hujitokeza tena na kuendelea kuzalisha vifungashio hivyo, lakini hata mamlaka husika nazo hubweteka kiasi cha kiwango cha uzalishaji na matumizi kuongezeka.

Mfano mzuri ni namna Serikali ilivyoendesha kampeni ya kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki kwa miaka ya hivi karibuni, ambapo vitisho vya adhabu kwa ambao wangebainika kuzalisha na kutumia mifuko na elimu kubwa iliyotolewa wakati huo, isingefikiriwa kuwa baada ya muda mfupi matumizi ya vifungashio hivyo yangerudi tena kwa kasi kubwa kiasi cha kuiamsha Serikali na kutangaza kampeni mpya ya kuzuia matumizi yake.

Hii ni dalili kuwa pamoja na dhamira ya Serikali kutotaka vifungashio hivyo, dhamira hiyo imekosa mikakati ya kiutekelezaji kiasi kuwa udhaifu huo unatoa mwanya kwa baadhi ya watu kuendelea na uzalishaji au kuagiza vifungashio hivyo kutoka nje.

Kwa Taifa kama letu ambalo baadhi ya maeneo elimu kuhusu vifungashio inaweza kuwa jambo gumu kwa wengi kuwafikia, dawa pekee si kutaka wananchi kuacha matumizi kwa kuwaeleza hatari yake, bali kunahitajika mkakati kabambe wa kuzuia kabisa uzalishaji, uingizaji na usambazaji wa vifungashio visivyo na sifa.

Wananchi ni kama bendera ambayo siku zote hufuata upepo. Serikali ikikaa kitako na wazalishaji, wasambazaji na wafanya biashara kwa jumla na kuweka mikakati ya kuzuia mianya yote ya kuwapo kwa vifungashio hivi, hatuoni namna wananchi kama watumiaji wa mwisho wanavyoweza kutumia vifungashio visivyo na sifa.

Tukidhibiti uzalishaji, hakuna namna kwa wananchi ila kutumia vifungashio vile vitakavyokubalika na Serikali kupitia mamlaka zake kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Tanzania ya uchumi wa kati unaochagizwa na maendeleo ya sekta ya viwanda, pamoja na mambo mengineyo inahitaji vifungashio. Hata hivyo, sheria inapaswa kufuatwa ili hatimaye tuwe katika nafasi nzuri ya kutunza mazingira kwa manufaa ya sasa na yale ya vizazi vijavyo.

Wito wetu ni kuwa pamoja na kufuata sheria, mamlaka husika zisimamie vilivyo wenye viwanda kuzalisha vifungashio ambavyo vinakidhi viwango, vinarejelezeka pamoja na kuwa na lebo ili iwe rahisi kumtambua mzalishaji na kudhibiti usambaaji wa vifungashio hivyo katika mazingira yetu.