TUONGEE KIUME: Kwa nini wanasema dunia duara?

Kuna muda nilipanga chumba cha kuishi Dar es Salaam. Asubuhi moja wakati nanyoosha shati langu ghafla umeme ukakatika; taa ikazimika, feni ikazimika, lakini ajabu ni pasi haikuzimika, bado ilikuwa inaendelea kuwaka.

Kwa haraka akili yangu ikanambia, hii itakuwa ni shoti ya umeme, sikuona sababu nyingine inayoweza kufanya ndani ya chumba kimoja, vyombo vingine vya umeme viwake na vingine vishindwe kuwaka.

Sasa hapa nikawa nawaza namna ya kutafuta fundi wa umeme kuja kuangalia tatizo. Lakini hali yangu ilikuwa ni mbaya, sikuwa na hela ya kumuita fundi kwa haraka namna hiyo, kwa hiyo ilinilazimu nisubiri siku mbili tatu.

Sikuweza kumwambia mwenye nyumba anirekebishie kwa sababu alikuwa ananidai kodi ya miezi kadhaa.

Sasa mtu hujamlipa kodi miezi miwili, unakwenda kumfuata kumwambia akurekebishie umeme ndani kwako? Una wazimu au kichaa?

Basi nikamaliza kunyoosha lakini nilipovaa tu kuna wazo likaja, linakaniambia nitazame mita yangu ya umeme.

Basi nilipofanya hivyo, nikagundua kuwa kumbe tatizo halikuwa shoti ya umeme, tatizo lilikuwa ni umeme ndani kwangu umeisha. Nikanunua umeme, nikaweka lakini nikabaki na swali kuhusu ule muujiza niliouona, wa umeme kuisha ndani kwangu lakini pasi kuendelea kuwaka.

Nikasema lazima nichunguze nijue imewezekana vipi.

Kupitia uchunguzi wangu nikaja kugundua kuwa kumbe ile swichi niliyokuwa natumia haikuwa ikitumia umeme wa chumba changu, ilikuwa inatumia umeme wa chumba cha upande wa pili, cha mpangaji mwingine kwa sababu zamani vyumba hivi vilikuwa ni chumba na sebule.

Basi tangu siku hiyo nikawa nafanya kila kitu kwenye hiyo swichi.

Kuchaji simu, TV, feni, pasi, kuchemsha maji, yaani matumizi yote ya umeme ambayo msela anakuwa nayo niliyafanya kwa umeme wa chumba cha pili kwa zaidi ya miezi sita.

Baadaye yule jirani yangu akahama na chumba chake kikabaki wazi kwa muda wa wiki kadhaa, siku moja nikiwa naongea na mpangaji mwingine akaniuliza, ‘hivi unajua kile chumba kilichokuwa wazi kinaingiliana umeme na chumba chako?’

Nikamjibu ‘hapana’ kwa sababu nilidhani kuwa na yeye anafahamu kwamba chumba changu kinaweza kutumia umeme wa chumba cha pili, ndiyo anataka kunipa hiyo taarifa.

Basi akaendelea akanambia; ‘Ndio hivyo bwana, kile chumba cha pili kinatumia umeme wa chumba chako, jamaa aliyehama alikuwa anatumia umeme wako siku zote.’

Nilichoka na hiyo ndiyo siku niliyojifunza kuwa kila baya unalomfanyia mwingine lazima litatafuta namna ya kukurudia.

Jamaa aliyekuwa anatumia umeme wangu na yeye umeme wake niliula, na mimi niliyekuwa nadhani napata mserereko kwa kutumia umeme wake, kumbe ndiye niliyekuwa mjinga zaidi, ameshakula umeme wangu siku zote hizo.