Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TUONGEE KIUME: Mwanaume kuwa na viwango

Kiwango cha wababa wanaoomba video za connection za watoto wa sekondari kwenye magrupu ya WhatsApp na mitandao mingine ya kijamii kinashangaza.

Ni hivi, wiki hii kulikuwa na uvumi kwamba kuna video za connection za watoto wa sekondari fulani Dar es Salaam zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii. Lakini kama unavyojua, video za aina hiyo zinapoingia kwenye mitandao ya kijamii ni ngumu kuzipata, inabidi uwe na connection, ufahamiane na watu, ndiyo maana zinaitwa connection.

Sasa wale ambao hawana connection wanakuwa kama matonya, ombaomba, wanazunguka kila mtandao wa kijamii kuomba video hizo. Mara waingie Twitter, “Hizo video ziko wapi jamani, na mimi naomba nizione.” Instagram, “Nani mwenye hizo video anitumie DM.” Huko kwenye magrupu ya WhatsApp ndo kabisa.

Kwa kawaida, tabia kama hizi zinafanywa zaidi na vijana. Siyo kwamba ni sawa vijana kufanya hivi, hapana, ila angalau umri wao unawabeba. Ujana upo karibu sana na utoto; ukiwa kijana unafanya vitu bila kujali, unaweza hata kufanya ujinga kwa sababu tu uonekane mjanja.

Lakini inapofikia hatua mwanamume mtu mzima anakuwa na tabia ya kuzunguka mitandaoni akitafuta video za connection, tena zinazodaiwa kuwa za mabinti wa sekondari, ni sawa na kusema tatizo limekuwa kubwa. Yaani mwanamume mtu mzima, unakuwaje na muda wa kuzurura kwenye intaneti ukisaka video za utupu za mabinti wenye umri sawa na watoto wako? Wadogo zako? Dada zako? Unataka kuona nini? Samahani kwa sentensi inayofuata, lakini kama unaona kuna kitu utakosa usipoona video hizo, mwambie binti yako basi akurekodie.

Maana moja ya kanuni niliyojifunza kwenye maisha ni kwamba, ukitaka kujua kitu ni kizuri au kibaya kukifanya, jiulize: Ingekuwa kinakutokea wewe ingekuwaje? Jiulize: Je, video unazotumia muda na bando kuzitafuta zingekuwa za mtoto wako, ungetumia nguvu hiyo hiyo?

Nilishasema siku moja hapa hapa, wanaokutwa na madhila ya video zao za faragha kuvuja kwa umma wanapaswa kupewa msaada, siyo kuzidi kuumizwa. Na mbaya zaidi ikiwa ni watoto. Wanaitwa watoto kwa sababu maalumu kwa umri wao bado wanajifunza, na katika kujifunza, kufanya makosa ni jambo la kawaida.

Ni muhimu pia kuzingatia athari za kijamii na kisaikolojia ambazo tabia hizi zinaweza kusababisha, si tu kwa wahusika waliomo kwenye video hizo, bali pia kwa jamii nzima. Matukio kama haya yanapochochewa na watu wazima, hasa wanaume, yanaimarisha utamaduni wa unyanyasaji wa kijinsia na kupunguza thamani ya utu wa wanawake na watoto wa kike. Mwanamume lazima uwe na viwango, bwana. Lazima kuwe na mambo ambayo useme, “Haya siwezi kuyafanya hata iweje.” Kuna tabia lazima uzikatae katakata, hata kwa kusingiziwa.

Fikiria mabinti zako wakigundua kwamba na wewe unaingia kwenye magrupu kutafuta video za connection.

Sana hata hizo salamu za heshima za shikamoo walizokuwa wanakupa, watataka kuzirudisha.

Kuwa mwanamume. Kuwa na viwango. Fanya mambo kama mwanamume.