TUONGEE KIUME: Ogopa kuwa aina hizi tatu za mwanamume
Ogopa sana kuwa mwanamume wa aina hizi tatu, mwanamume asiyekuwa na pesa, mwanamume asiyeweza kuongoza hisia zake na mwanamume mwenye akili za ujana.
Ogopa kuwa mwanamume asiyekuwa na pesa kwa sababu pesa ndiyo nguvu ya enzi hizi. Pesa ni sabuni ya roho. Pesa ni kila kitu. Ukiwa na pesa kuna uwezekano mkubwa wa wewe na familia yako kuishi peponi mkiwa duniani.
Mkiumwa mtakwenda hospitali nzuri, mtakula chakula chochote mnachotaka, mtaishi sehemu nzuri. Kwa kifupi pesa haihitaji kuelezewa sana, umuhimu wake unajieleza.
Ishu ni kwamba, njia za kuwa mwanamume mwenye pesa haziko wazi, kwa mfano, wengine watakwambia ufanye kazi kwa bidii, lakini sio kila aliyefanya kazi kwa bidii ameishia kuwa mwanamume mwenyewe pesa. Ni kama vile hatujui mtoa riziki anatoa riziki kwa kuzingatia nini. Kwahiyo pengine njia kuu zaidi ya kujikwamua hapa ni kufanya kazi na kuomba mtoa riziki atukumbuke ili tusiwe wanaume tusiokuwa na pesa.
Pili, ogopa kuwa mwanamume asiyeweza kuongoza hisia zake kwa sababu kila kinachotokea kwenye maisha yako ni matokeo ya hisia zako.
Wanafalsafa wanasema, maisha ya mwanadamu ni asilimia 10 mambo yanayotokea, na asilimia 90 jinsi unavyopokea mambo yanayotokea. Na upokeaji wako wa mambo unategemea uwezo wako wa kuongoza hisia zako.
Kwa mfano kiongozi wako ofisini amekuwa akikukosoa kwa kukuonea. Na maoni yake juu yako yanaweza kuhatarisha hata kibarua chako.
Kama mtu anaweza kudhibiti hisia zake, anaweza kutambua kwamba kujibu kwa hasira hakutasaidia. Badala yake, anaweza kujibu kwa utulivu, labda kwa kuuliza maswali ya kujenga au kutafuta ufafanuzi zaidi.
Njia hii inaweza kuleta maelewano na hata kufungua majadiliano yenye tija zaidi na kiongozi wake, kumsaidia kukua na kujijengea sifa nzuri ofisini.
Kwa upande mwingine, kama ni mtu asiyeweza kuongoza hisia zake ataacha hisia zimuongoze; anaweza kujibu kwa hasira au kujihami. Hii inaweza kuharibu uhusiano wake wa kikazi na sifa yake, na hata kupelekea hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi yake.
Katika mfano huu, matokeo yote yanatokana na tukio lilelile kukosolewa. Lakini matokeo ya mwisho yanategemea jinsi anavyodhibiti na kuongoza hisia zake.
Mwisho, ogopa sana kuwa mwanamume mwenye akili za ujana kwa sababu ujana na ujinga ni kama uji na mgonjwa. Fikiria, ni wakati gani katika maisha yako ulifanya vitu vya kipuuzi zaidi kuliko ujana?
Ulijifunza kunywa pombe ukiwa kijana, ulijifunza kuvuta bangi au shisha ukiwa kijana, ulijifunza mambo yote mabaya ukiwa kijana na hata ukiulizwa kwa nini hata ulitamani kujifunza mambo hayo unaweza usiwe na majibu.
Sasa vuta picha akili hiyo uendelee kuitumia ukiwa mwanamume mtu mzima. Maana yake utakuwa unafanya mambo ya kufanya watu wakuite mtu mzima hovyo.
Mfano, mkasa unazungumziwa zaidi kwa sasa kwenye mitandao ya kijamii unaomhusu mwanamume kutoka nchini Equatorial Guinea aitwaye Bartazary Engonga, aliyetembea na wanawake 400 na kuwarekodi video, wengi wakiwa ni wake za watu, ni mfano wa watu wazima wenye akili za ujana.
Yaani unafanya usaliti na wake za watu ofisini na kujirekodi video na kuzitunza. Niambie kipi kati ya hayo hakitoshi kuwa uthibitisho wa ujana ni ujinga? Sasa vuta picha uwe mwanamume mwenye akili za ujana.