Tushirikiane kuzuia dawa za kulevya nchini

Muktasari:

  • Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa kwenye mapambano ya kudhibiti uuzaji, uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya ambazo zimeleta athari kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa kwenye mapambano ya kudhibiti uuzaji, uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya ambazo zimeleta athari kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Miongoni mwa jitihada hizo ni kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya na kuajiri watu wenye sifa stahiki.

Viongozi mbalimbali, akiwamo Rais wa tano hayati John Magufuli walivalia njuga suala hilo kwa kuimarisha Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya ili Taifa lisipoteze nguvukazi inayoathirika matumizi ya dawa hizo.

Kimsingi, watumiaji wakubwa wa dawa hizo ni vijana ambao ndiyo nguvukazi. Vijana waliotopea kwenye utumiaji wa dawa hizo mwisho wake hugeuka ‘mateja’ ambao bila dawa hizo hawawezi kufanya shughuli zao.

Watu wenye uraibu (watumwa) wa dawa za kulevya hukosa hamu ya kula, hali inayosababisha miili yao kudhoofu na kukosa nguvu, hivyo kuathiri mwenendo mzima wa maisha yao na uzalishaji mali.

Mtu wa aina hii huwa mzigo kwa familia na taifa. Gharama kubwa hutumika kumpa tiba ya kuacha kutumia dawa hizo. Wengine hupoteza maisha au uwezo wa kufikiri na kutenda mambo sawia.

Tunajua vita ni ngumu kwakuwa wanaojihusisha na biashara hii ni watu wenye nguvu za kimadaraka na kiuchumi. Hata hivyo, tunahitaji nguvu ya pamoja kushinda vita hii.

Tunafarijika kila mara tunaposikia au kuona taarifa za watu kukamatwa, kushtakiwa na kuadhibiwa kutokana na kujihusisha na matumizi, uingizaji au usafirishaji.

Juzi Kamanda wa Polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Jeremia Shila alitoa taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa wawili wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kilo 13.4 wakiwa safarini kuelekea nchini India baada ya kutoka Zimbabwe.

Watuhumiwa hao walikuwa kwenye mashine ya ukaguzi wa mizigo tayari kwa safari, lakini kutokana na ubora wa vifaa vya ukaguzi walibainika.

Ni jambo jema kwa Taifa kuwa na vifaa vya kisasa vya ulinzi na utambuzi wa vitu hatari vinavyoweza kuleta athari zaidi kama vitasafirishwa nje ya nchi au kuingizwa nchini.

Tunaamini uwekezaji kwenye vifaa vya kisasa unaendaana na kuwaweka watu waadilifu kwenye maeneo nyeti ili nchi iendelee kubaki salama.

Tunapongeza jitihada za kukamata dawa za kulevya na watuhumiwa wake, lakini tungependa ulinzi uongezwe zaidi katika mipaka, bandari, stendi za mabasi na njia za vichochoroni.

Tunaamini watumiaji, wauzaji na wasafirishaji wanajulikana kwa kuwa wanaishi kwenye jamii, hivyo ni jukumu la jamii kuwafichua ili wachukuliwe hatua za kisheria zitakazosaidia kukomesha biashara hii haramu.

Usiri, kulindana na rushwa vimechangia kukua kwa biashara hii. Vyombo la dola navyo viwalinde na kuheshimu usiri wa watoa taarifa za biashara hii haramu badala ya kuzitumia taarifa hizo kutafuta masilahi binafsi.

Tunaomba pia mahakama na wachunguzi wafanye kazi zao kwa haki na kufuata sheria ili kukomesha biashara hii. Uwezo wa kuzuia utumiaji, usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya tunao.

Tushirikiane kufikia Tanzania tunayoihitaji ikiwa na watu wenye afya bora watakaoweza kuzalisha mali zitakazomsaidia mtu mmoja mmoja na Taifa.

Jamii isitegemee vyombo vya dola pekee kufanya kazi ya ulinzi, kwa kuwa idadi ya watendaji kwenye vyombo hivyo haitoshi; kila mmoja wetu awe mlinzi na atoe taarifa anapobaini nyendo zisizofaa miongoni mwa majirani zake.