Tutafute muafaka, maridhiano kabla ya Uchaguzi Mkuu

Kwa Mtanzania yeyote anayefikiri sawa na anayeitakia mema nchi yetu, atakubaliana na mimi nchi iko katika mtanziko kutokana na kile kilichojitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na 2024 na uchaguzi mkuu 2020.
Mtanziko huo ndio unaonisukuma kuona upo umuhimu wa nchi yetu kutafuta muafaka na maridhiano ya kitaifa na kuisuka upya mifumo ya kisheria ya uchaguzi, kama kweli tunataka kuwa na uchaguzi huru na haki 2025.
Ukisoma taarifa ya taasisi ya International Peace Insitute (IPI) ya mwaka 2011, inaonyesha kati ya 1990 na 2010, nchi zilizokuwa zikifanya uchaguzi wa kidemokrasia katika bara la Afrika ziliongezeka kutoka asilimia saba hadi 40.
Kwa Tanzania, chaguzi ambazo zilikuwa na minong’ono kidogo ni uchaguzi mkuu 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015, lakini chaguzi zilizofuata tulianza kushuhudia vituko na vioja katika chaguzi tofauti.
Katika chaguzi hizo za kuanzia 1995 hadi 2015, angalau tuliruhusu waangalizi wa ndani na wa kimataifa, mawakala wa vyama vya siasa walitekeleza majukumu yao pasipo kubughudhiwa na wala hatukushuhudia uenguaji mkubwa wa wagombea.
Vyama vya siasa na wagombea walishindana kwa sera na hata matokeo yaliakisi ushindani huo, kwani hata 2015 mgombea wa CCM, John Magufuli alipata kura asilimia 58.46, huku mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa akipata asilimia 39.97.
Ukiangalia Uchaguzi Mkuu wa 2010, mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete aliibuka na ushindi wa asilimia 61.17, Dk Wilbroad Slaa wa Chadema akipata asilimia 26.34 na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF akipata asilimia nane ya kura zote.
Huo ndio ulikuwa mwelekeo wa kukua kwa demokrasia, lakini ghafla uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, nchi ikashuhudia maelfu ya wagombea wa vyama vya upinzani nchi nzima, wakienguliwa kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kutojua kusoma na kuandika.
Ni uchaguzi huo dunia ilishuhudia CCM ilishinda kwa karibu asilimia 99, huku ikizoa mitaa yote 4,262 nchini na katika uchaguzi huo baadhi ya wagombea wa CCM kupita bila kupingwa katika vijiji 12,028 na vitongoji 62,927 Tanzania Bara.
Uchaguzi Mkuu 2020 ndio nchi ikaendelea kushuhudia kuibuka kwa magenge ya kihalifu yaliyoteka baadhi ya wagombea wa upinzani, kuwatesa, kuwapora fomu za kugombea, kutesa wafuasi wa vyama vya upinzani na mawakala kutimuliwa vituoni.
Ni kupitia uchaguzi huo, mgombea urais wa CCM, John Magufuli alipata kura asilimia 84, akifuatiwa na mgombea wa Chadema, Tundu Lissu kura asilimia 13 na Benard Membe wa ACT-Wazalendo akiambulia asilimia 0.5 ya kura zote.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 haukuwa na tofauti na ule wa 2019 ambapo CCM iliibuka na ushindi wa asilimia 99.01 kwenye nafasi za wenyeviti wa vijiji, asilimia 98.26 kwenye nafasi za wenyeviti wa vitongoji na asilimia 98.8 ya wenyeviti wa mitaa.
Nimetumia muda mrefu kueleza tulipotoka, tulipo na sasa nitaeleza tunapotaka kwenda kama taifa letu lenye watu wanaojitambua.
Ni mwelekeo huo wa uchaguzi wa kuanzia mwaka 2019, ndio ambao umekifanya chama kikuu cha upinzani nchini cha Chadema kuja na msimamo mkali kuwa pasipo mabadiliko ya mifumo, basi hakutakuwa na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani 2025.
Katika kuridhiana na kutafuta muafaka huo wa kisiasa, ni lazima tukubaliane kuwa kwa mazingira tuliyopitia, tunahitaji Tume Huru ya Taifa yenye sifa ya kuwa huru na siyo jina, na tunahitaji mifumo ya kisheria ya uchaguzi ambayo ni shirikishi.
Ni lazima mifumo yetu ya uchaguzi ihakikishe hakuna mizengwe kwenye uandikishaji wapigakura, uteuzi wa wagombea, kampeni, upigaji kura na utangazaji matokeo na kwamba aliyeshinda ndiye pekee anatangazwa mshindi na si vinginevyo.
Udanganyifu wowote ule unaolindwa na mifumo katika upigaji na uhesabuji kura katika uchaguzi mkuu 2025 unaweza kuiingiza nchi kwenye machafuko, hivyo ni lazima kabla ya kuufikia uchaguzi mkuu, dosari zote nilizozieleza zipatiwe majibu.
Nataka niseme, dhamana ya amani ya nchi hii ipo mikononi wa Serikali ya CCM na wanapaswa kuishi katika kauli ya Napoleon Bonaparte, aliyepata kuwa mtawala wa Ufaransa aliyeonya kuwa watu unaokosana nao na wakakaa kimya ni hatari sana.
Siku zote moyo una kikomo cha uvumilivu, tusiwafikishe Watanzania huko hadi baadhi wajione kuwa wanachukuliwa kama wao ni raia wa daraja la pili, hatutabaki salama kamwe na tutambue hakuna mtu, kiongozi au chama chenye hati miliki ya kuongoza nchi.
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba 0656600900