Twende zaidi ya leseni maduka kubadili fedha

Twende zaidi ya leseni maduka kubadili fedha

Muktasari:

  • Kauli ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kwamba ifanyike tathmini na kuwarudishia leseni wamiliki wa maduka ya kubadilishia fedha waliofungiwa maduka, ni ya matumaini. Ni moja ya hatua za kuponya vidonda katika Sekta Binafsi katika eneo la biashara na uwekezaji.

Kauli ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kwamba ifanyike tathmini na kuwarudishia leseni wamiliki wa maduka ya kubadilishia fedha waliofungiwa maduka, ni ya matumaini. Ni moja ya hatua za kuponya vidonda katika Sekta Binafsi katika eneo la biashara na uwekezaji.

Katika mahojiano yaliyoibua kauli hiyo aliyoyafanya na kituo cha televisheni cha Azam TV, Dk Mwigulu ameagiza pia kuangaliwa kiwango cha mtaji kinachotakiwa ili kuanzisha biashara ya kubadilisha fedha ili kumaliza malalamiko aliyoyapokea kutoka kwa wanaofanya biashara hiyo.

Kilichoibua swali na majibu hayo ni hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusu maduka ya kubadilishia fedha yaliyofungwa mwaka 2019 baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufuta leseni za maduka hayo na malalamiko yaliyoambatana na hatua hiyo kwamba fedha za wamiliki wa maduka hayo zilichukuliwa na Serikali na kiwango vya mtaji vikaongezwa hadi hatua isiyofikiwa na wengi na hivyo kuwatoa kwenye mchezo.

BoT iliendesha operesheni maalumu ya kufunga maduka hayo hasa katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha na baada ya operesheni hiyo, shughuli ya kubadilisha fedha za kigeni ilielekezwa kwenye benki za biashara na kubakiza maduka machache.

Kwa vyovyote hatua ya Dk Mwigulu ya kuagiza wafanyiwe tathmini ili waendelee na biashara hiyo ni njema na ya kufurahiwa na kila mpenda haki, japokuwa ingekuwa njema na yenye matumaini zaidi endapo ingezungumzia pia utaratibu wa kurejesha fedha zilizochukuliwa kinyume na utaratibu kwa waliokuwa wanamiliki maduka hayo, ili wapate mitaji na nguvu za kuanza kazi upya.

Bila shaka kwa kuwa Dk Mwigulu amekutana na wafanyabiashara hao na kuzungumza nao, watakuwa wamemweleza kilio cha kupokwa mitaji yao, kama ambavyo wamekuwa wakikitoa kwa njia mbalimbali kabla ya Serikali ya sasa haijaingilia kati suala lao.

Ni hivi karibuni katika mjadala wa Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa na Mwigulu mwenyewe bungeni, baadhi ya wabunge akiwemo wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo walipaza sauti za wafanyabiashara hao, wakiweka wazi jinsi walivyoporwa fedha zao na kutoa wito fedha hizo zirejeshwe.

Ingawa hata Gambo mwenyewe alikosolewa kwamba wakati fedha hizo zinachukuliwa ndiye alikuwa mkuu wa mkoa Arusha, lakini hoja ya msingi kwa sasa ni fedha za wafanyabiashara kuchukuliwa isivyo halali, bila kuangalia nyuma kutafuta lilikuwa agizo la nani.

Kutokana na wito huo wa kurejesha fedha tunaamini hata Dk Mwigulu ataendelea kulitafakari suala hilo ili limalizwe kwa ukamilifu wake, ikiwezekana hata kulipa fidia kwa uharibifu uliofanywa.

Ni maoni yetu kwamba suala hilo halitaishia hapo, bali litakwenda hadi kwenye sheria na kanuni kama kuna mpya zilizotungwa kuhalalisha kilichofanyika zifutwe ili mazingira ya kufanya biashara yaendelee kuboreshwa ili suala kama hilo isitokee tena kwa siku zijazo.

Pamoja na hoja ya Mwigulu kwamba kulikuwa na matatizo ya kisera ambapo kwenye baadhi ya maeneo ungeweza kukuta maduka yamepangana na mengine yana fedha nyingi kuliko hata kwenye benki, tunadhani hilo linazungumzika na leseni zinaweza kutolewa kulingana na maeneo, lakini si kwa kuyafunga wala kuchukua fedha zilizo katika maduka.

Busara ambazo zimetumika katika hatua hii ya kuzungumza na kuanza kutoa leseni, ziendelee hadi katika kurejesha fedha na mitaji kwa wale watakaobainika walitendewa isivyo.