UCHAMBUZI: Wanasoka wa kigeni si maadui, tusiwachukie

Muktasari:

  • Katika takwimu za ufungaji, Simba, Yanga na Azam ndizo timu ambazo zimefunga idadi kubwa ya mabao lakini asilimia kubwa ya mabao hayo yamepachikwa na wachezaji wa kigeni huku yaliyobakia ndio yakiwekwa kimiani na wazawa.

Ni raundi tisa zimesalia kabla ya Ligi Kuu ya NBC msimu huu kumalizika huku Yanga wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi na pointi zao 56 huku Simba yenye pointi 48 ikiwa nafasi ya pili na pointi 48 na nafasi ya tatu inashikiliwa na Azam FC yenye pointi 43.

Wakati ligi ikielekea ukingoni, tathmini ya takwimu tofauti inaonyesha kuwa wachezaji wa kigeni bado wameendelea kufanya vizuri na kuwa na mchango mkubwa katika timu zao.

Na hili halijatokea kwa bahati mbaya kwani katika timu nyingi ambazo zina wachezaji kutoka nje ya Tanzania, nyota hao wamekuwa na uhakika wa nafasi katika kikosi cha kwanza jambo linalowaweka katika nafasi nzuri ya kuwa na takwimu hizo bora.

Katika takwimu za ufungaji, Simba, Yanga na Azam ndizo timu ambazo zimefunga idadi kubwa ya mabao lakini asilimia kubwa ya mabao hayo yamepachikwa na wachezaji wa kigeni huku yaliyobakia ndio yakiwekwa kimiani na wazawa.

Kwa Yanga imekuwa ikimtegemea zaidi Fiston Mayele katika kufumania nyavu na ndio anaongoza kwa kufunga katika Ligi Kuu akiwa na mabao 15 na anayemfuatia ni Moses Phiri wa Simba mwenye mabao 10 wote wakiwa ni wageni.

Orodha ya makipa ambao wamecheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa (clean sheet), kinara wake ni mlinda mlango wa Yanga kutoka Mali, Djigui Diara akifuatiwa na Aishi Manula ambaye ni mzawa.

Ukitazama kwa upande wa wachezaji waliopiga pasi nyingi za mabao, kinara ni Mzambia Clatous Chama aliyepiga pasi 12 za mwisho akifuatiwa na nyota kutoka Burundi, Saido Ntibazonkiza ambaye yeye amepiga pasi nane (8) zilizozaa mabao.

Takwimu hizo bora za wageni zinathibitisha wazi kuwa ni wachezaji muhimu katika timu zetu kutokana na mchango wanaoutoa ambao pengine kama wasingekuwepo, ni wazawa wachache wangeweza kufanya hivyo.

Uwepo wao unaongeza mvuto na hamasa ya ligi na hata kuimarisha ubora wa timu na ndio maana sio jambo la kushangaza tangu timu zetu zlipoanza kuwa na namba kubwa ya wachezaji wa kigeni, tumeona zikichomoza na kuleta ushindani mkubwa katika mashindano ya klabu Afrika.

Kwa maana nyingine, kutikisa kwa wageni katika Ligi Kuu inayoendelea, kunafuta taratibu ile dhana kwamba wachezaji wa kigeni wanapokuja kwa wingi, wanaathiri maendeleo ya wachezaji wazawa na kuzorotesha viwango vyao.

Wapo wanaofikia hatua ya kuhoji na kushangazwa na kitendo cha klabu kulipa mishahara mikubwa kwa wachezaji wa kigeni kulinganisha na wale wazawa na hii kwa namna fulani inachangia kutengeneza chuki baina ya wazawa na wageni.

Hata hivyo wanasahau kwamba kinachowasaidia wachezaji wa kigeni hadi wanachota fedha nyingi za timu zetu na kupata uhakika wa kucheza mara kwa mara ni juhudi kubwa binafsi ambayo wamekuwa wakiifanya katika mechi na viwanja vya mazoezi ili kuwapa makocha wao sababu ya kuwapanga vikosini.

Kwa upande mwingine wamekuwa makini katika kusimamia maslahi yao kabla ya kusaini mikataba ya kutumikia timu hizo kwa kuweka mkazo wa uwepo wa vipengele ambavyo vitawanufaisha wao kifedha na stahiki nyingine.

Hii ni tofauti kwa wachezaji wazawa ambao wengi wanashindwa kuonyesha jitihada kubwa mazoezini na hata wanapopata nafasi katika mechi jambo ambalo linakatisha tamaa makocha kuwapa fursa kwa mara nyingine wakiamini kwamba watawaangusha.

Lakini pia hata katika nyakati za usajili, wachezaji wazawa huamini kuwa kuwa klabu zinawasajili kwa hisani na sio kutokana na viwango vyao jambo linalopelekea kuwa na mikataba inayowabana na kutowanufaisha.

Suluhisho la haya ni kwa wachezaji wazawa kufanyia kazi kile ambacho wenzao wamekuwa wakikifanya kwa ajili ya maslahi yao binafsi na sio kujihisis kuwa wakifanya hivyo wataonekana kama wanazisaliti timu.

Watumie fursa ya kuwepo kwa wageni kukaa nao karibu na kujifunza mambo ambayo yanachangia kuwafanya wafanikiwe nje na ndani ya uwanja badala ya kujitenga nao na kuhisi uwepo wao unawabania ridhiki zao.

Hilo ndilo jambo pekee ambalo linaweza kutusaidia zaidi badala ya kujenga chuki ambazo haziwezi kuwa na msingi, kwani kuna wageni wana uwezo mkubwa na wanaweza kuwa darasa zuri kwa wazawa badala ya kuwaza tofauti juu yao.