Vitendo hivi vya Polisi havikubaliki

Muktasari:


Jukumu kubwa la Polisi ni kulinda raia na mali zake, unapokuta askari anafanya tofauti na miongozo, sheria na taratibu hapaswi kuvumiliwa kwa kuwa anaichafua taasisi mbele ya jamii.

Kitendo kilichofanywa na askari polisi wawili kuingia kwenye nyumba ya starehe na silaha za moto kisha kutuhumiwa kusababisha kifo cha mlinzi wa baa ya Board Room iliyopo Sinza jijini Dar es Salaam, hakipaswi kuvumiliwa.

Ni jambo jema watuhumiwa hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi, jamii ingependa kuona haki inatendeka kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria.

Tunajua kuna taratibu za kufuatwa kama askari wanashuku eneo fulani kuna watuhumiwa, lakini matumizi ya silaha sehemu isiyostahili ni kuonyesha bado kuna askari wasiotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi, mafunzo na kiapo chao.

Katika mazingira tuliyonayo, askari wanakwendaje baa wakiwa na silaha kwa madai ya kusaka wahudumu wanaodaiwa kujiuza? Tunaamini uchunguzi huu utawezesha watuhumiwa kufikishwa mbele ya sheria lakini pia utatoa funzo kwa askari wengine wanaokwenda na silaha maeneo yasiyostahili.

Tunajiuliza askari anapokwenda kwenye sehemu ya ulevi na silaha ikitokea kanyang’anywa na ikaenda kutumika kwenye uhalifu, atajibu nini kwa taasisi iliyomuajiri na kumpa silaha?

Tunafahamu Jeshi la Polisi ndio chombo kilichopewa mamlaka ya kulinda usalama wa raia pamoja na mali zao, ikiwamo kupambana na uhalifu, kukamata wavunja sheria, lakini pia kulinda raia na mali zao.

Hata hivyo, baadhi ya askari polisi wamekuwa kikwazo cha kutekeleza lengo kuu hilo la jeshi la kulinda raia na mali zao, wamegeuka kuwa adui wa raia kwa kuwapa vitisho ikiwamo matumizi ya nguvu na silaha pasipo sababu.

Tukio la Sinza ni mwendelezo wa vitendo vinavyofanywa na baadhi ya askari polisi wasio na nidhamu ya kazi na kuwafanya wananchi wawaone askari polisi kama maadui, na si rafiki wa kushirikiana nao kupambana na uhalifu.

Askari wanaongozwa na Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi (Police General Orders) au kwa kifupi PGO, ambazo zinawataka wafanye kazi zao kwa weledi bila kuonea mtu.

Kuna wakati Rais Samia Suluhu Hassan aliwahi kunukuliwa akisema wimbo wa polisi siku zote ni kufanya kazi kwa uzalendo, weledi, bidii, uaminifu na uadilifu, lakini alisema atashangaa kuona askari polisi wanakengeuka maneno hayo.

Tunasikitika kuona baadhi ya askari polisi wakishindwa kufanya kazi zao kwa weledi na umakini na badala yake kuishia kutumia nguvu bila sababu.

Kitendo kilichofanywa na askari hao wawili kwenye nyumba ya starehe Sinza kinasikitisha na tunakilaani na kukikemea kwa nguvu.

Inatia aibu kwa askari aliyehitimu mafunzo chuoni kushindwa kujua ni eneo gani na kwa mtu gani anapaswa kutumia nguvu kubwa kumdhibiti raia asiyekuwa na silaha wala hatia.Kitendo hicho cha kutumia silaha ya moto hakikubaliki, pia kinaonyesha wazi jinsi Watanzania tusivyo salama mbele ya walinda usalama.