Wasanii tupambanie uhai, tusisubiri kuomboleza

Wiki moja iliyopita, tasnia ya muziki wa kizazi kipya ilipata pigo baada ya kufariki kwa msanii wake Haitham Ghazal Seif maarufu kwa jina la ‘Haitham King’.

Msanii huyo miezi miwili iliyopita aliachia kibao chake cha ‘Hakutaki’ kilichoanza kufanya vizuri katika mitandao mbalimbali ya kuuzia muziki ,tv na vituo vya redio.

Nyota yake ni kama ilianza kung’ara kupitia wimbo huo licha ya kwamba alianza kuimba miaka saba iliyopita.

Vibao vingine alivyowahi kuimba enzi za uhai wake ni pamoja na ‘I wish’, ‘Ukaniumiza’, ‘Ex Mtamu’, ‘Huba’, ‘Utamu’ na ‘Come Over’.

Haitham aliyekuwa mama wa mtoto mmoja, alifikwa na umauti akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Temeke.

Kwa mujibu wa mumewe, Brayson alisema marehemu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la upumuaji ambalo lilianza kama homa ya kawaida, lakini baadaye akawa anakosa pumzi hadi kuwekewa mashine ya kumsaidia kupumua na kulazwa katika chumba cha uangalizi maalumu hadi alipofikwa na umati.

Baadhi ya wasanii na watu maarufu walitumia kurasa zao kuomba msaada wa michango ili kuokoa maisha yake, ambapo ilielezwa zilikuwa zinatakiwa Sh5 milioni kwa ajili ya matibabu yake.

Mmoja wa wasanii walisaidia kusambaza tangazo hilo ni Ali Saleh, maarufu Alikiba licha ya baadhi ya watu kulipokea kwa mtazamo tofauti, huku wengine wakilaumu kuwa wasanii hawana tabia ya kujiwekea akiba na wanapoumwa wanaanza kuomba michango.

Binafsi naona watu hao hawakuwa sahihi kwani hakuna anayeomba kuumwa na huwezi kujua mpaka wanafika hatua ya kukubali kutangaza kuomba mchango wameshatumia gharama kiasi gani.

Hata hivyo hiki sicho nilicholenga kusema bali nimeguswa kueleza kuhusu wasanii namna wanavyopokea changamoto za wenzao.

Nilidhani baada ya kutoka tangazo la Haitham kuhitaji matibabu wao wangekuwa mstari wa mbele kuchanga na kupokezana kulisambaza ili lifike mbali, lakini haikuwa hivyo kwa baadhi yao.

Tena nilipata ukakasi hata kuliona kwa sababu ninajua kwa baadhi ya wasanii Sh5 milioni ni fedha ndogo au hata wangejikusanya na kuchangishana ingetimia mapema sana.

Nakubali kifo ni mipango ya Mungu, lakini wengine hufa kwa kukosa matibabu. Hata bendi ya DDC Mlimani Park, maarufu Sikinde waliwahi kuimba ‘Huruma kwa wagonjwa’ wakisisitiza umuhimu wa kuwasaidia wagonjwa badala ya kusubiri kuomboleza kwa mbwembwe nyingi.

Ajabu ni katika kipindi hicho wasanii wengi walionekana kujikausha kama hawana taarifa ya kinachoendelea juu ya kuumwa kwa Haitham.

Sasa siku chache baada ya taarifa kusambaa ya kifo chake, ilikuwa kila ukurasa wa msanii unaopitia ni RIP Haitham, mpaka unajiuliza wakati anaumwa kwa nini hawakuonyesha huruma hii kwa vitendo kuokoa maisha yake.

Katika hili wasanii mnapaswa kubadilika kwani hakuna anayeijua kesho yake, na katika ugonjwa haijalishi una hela kiasi gani pia inaweza kukata ukiwa bado unaugua.

Lakini ndio ubinadamu huo kusaidiana kwenye shida na raha na ndio kipindi cha kuondoa tofauti mlizonazo.

Maisha yenu wasanii yasiishie ia kwenye kula bata pamoja, lakini pia muangalie na mtu anapopatawa na tatizo kama hili la ugonjwa.

Lakini kubwa na la kujifunza kila mmoja wenu anatakiwa kujitolea pale kunapokuwa na tatizo linalowahusu, ili kesho isije mtu akasaidia kwa sababu ni mtu wa karibu wa fulani.

Yaani namaanisha kuleta utimu kwenye kunusuru uhai. Uhai kwanza mengine yanafuata.

Hizi timu huyu anamuunga mkono yule zinatokana na uhai na kuwa na afya njema, nje ya hapo tunategemeana sana hasa wakati wa kupambania afya zetu.

Inajulikana kulikuwa na watu wa watu, lakini waliumwa kiasi cha kuchangiwa sirini na mwishowe hadharani, hivyo tusaidiane tukilitambua hili. Kwamba nasi ni wagonjwa watarajiwa na tutahitajiana kama siyo hapa, pale.

Inapotokea mmoja wenu ana changamoto liwe ni jukumu lenu wote badala ya kukaa kimya na kuendekeza mambo ya starehe.

Pia wasanii na nyinyi ni binadamu na mnafikwa na changamoto hasa za maradhi, jiandaeni kwa kujikatia bima ya afya.

Natambua kuna maardhi matibabu yake hayako kwenye bima, ila yale yanayotibika muwe na uhakika wa matibabu yake.

Mbali an bima, pia jipangeni kwa ajili ya maisha yajayo, sikatai msile bata kwani ndiko waliko wateja wa kazi zenu, ila msijisahahu sana.

 Baadhi yenu hawana nyumba zao wenyewe, lakini wamepanga mahekalu wanalipa kodi kubwa, wanasahau sanaa huendana na umri, itafikia mahali wataachana nayo na kulazimika kufanya vitu vingine na pengine kipato chao kitapungua pia.

Busara ni kutumia vema wakati wa sasa ambapo kazi mnazofanya zinawalipa kujiandaa kwa ajili ya baadaye, kuliko kuendekeza anasa.

Nasisitiza bima ya afya ni muhimu kwa kila Mtanzania mkiwemo nyinyi wasanii, maradhi humpata yeyote.