Chama, Kagere watengewa mamilioni, Platinum kazi wanayo...

SIKU nne tu kabla ya kuvaana na FC Platinum ya Zimbabwe katika pambano la marudiano la Ligi ya Mabingwa Afrika, Clatous Chama, Luis Miquissone na nyota wengine wa Simba wametengewa mamilioni ya fedha watakayovuna iwapo watawang’oa Wazimbabwe hao.

Simba itakuwa wenyeji wa Platinum katika mechi itakayopigwa Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, huku wakiwa na kazi ya kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 ugenini, ili kujihakikisha wanatinga hatua ya makundi kwa mara yao ya tatu.

Wekundu hao wa Msimbazi walitinga hatua hiyo ya makundi ya ligi hiyo mara ya kwanza 2003 na 2018-2019, na kwenye mechi yao dhidi ya Wazimbabwe wanahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili kupindua meza na kusonga mbele, huku wakibebwa na rekodi zao kwenye uwanja wa nyumbani.

Katika kuhakikisha wanatinga hatua hiyo, mabosi wa Msimbazi wameamua kuwatia mzuka kina Chama kwa kuwaahidi mamilioni ya fedha kama wataing’oa Platinum.

Ipo hivi. Mara baada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara kumalizika kwa Simba kushinda mabao 4-0 dhidi ya Ihefu, Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez akiwa sambamba na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Dk Mohammed Janabi waliwavamia nyota wao na benchi la ufundi katika chumba cha kubadilishia nguo na kuteta nao kwa muda mfupi.

Barbara na Janabi kabla ya kuingia katika chumba hicho walifanya kikao kifupi na kocha Sven Vandenbroeck, japo Mwanaspoti halikubaini walichokizungumza, lakini mwisho wa tukio hilo kila mmoja alicheka na kumwambia mwenzake safi sana.

Baada ya hapo Janabi na Barbara waliingia katika chumba cha kubadilishia nguo na kuzungumza na wachezaji, kwanza kwa kuwapa hongera kwa kazi kubwa ya ushindi wa mabao tisa ndani ya michezo miwili iliyopita na mwisho wa maongezi yao walitoa ahadi ya mamilioni hayo ya fedha.

Inadaiwa wachezaji hao waliahidiwa kupewa Sh250 milioni ili wagawane iwapo tu wataitupa nje ya michuano Platinum iliyo na nyota kama Perfect Chikwende na Mtanzania Elias Maguri, taarifa inayoelezwa iliwapa kina Chama furaha na kuahidi kuwamaliza Wazimbabwe.

Mmoja wa waliokuwa kwenye kikao hicho kifupi, aliliambia Mwanaspoti kwamba wachezaji na benchi la ufundi walionekana kuwa na furaha kwa ahadi hiyo ya mamilioni na akili za nyota hao wa Simba ni kuhakikisha hawapishani na fedha hizo.

“Sh250 milioni zilizoahidiwa na viongozi ni pesa nyingi kwa maisha ya kibongo kiukweli imeongeza morali kwa wachezaji ya kushindana zaidi pengine tofauti na ilivyokuwa katika mechi ya kwanza. Tumepania kupambana hadi jasho la mwisho ili tushinde na tubeba mkwanja huo,” alisema mmoja wa mjumbe wa kikao hicho aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.

Mbali na mzuka huo waliopewa wachezaji na benchi la ufundi, pia kina Barbara na Dk Janabi walisikika wakiwa nje ya chumba hicho wakiwapa maneno ya morali na motisha makomandoo wa Simba ambao nao walionekana kuwa na furaha kwa kauli za mabosi wao hao.

Mwanaspoti lilijaribu kuwasiliana na Barbara ili kuthibitisha juu ya ahadi hiyo, lakini simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa, hata hivyo Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Abdallah Salim ‘Try Again’ alipoulizwa alisema suala la ahadi ya motisha kwa wachezaji ni jambo la kawaida.

“Simba tuna utamaduni wa kuwapa motisha wachezaji wetu kwa kila mechi zinazoonekana kuwa ngumu na muhimu, ila mpaka sasa hakuna kiwango kilichowekwa wazi, lakini ni kwamba wachezaji wanajua ahadi ipo na kazi inabaki kuwa yao uwanjani,” alisema Try Again kwa kifupi.

Alipobanwa zaidi, Try Again alisema ahadi itatolewa kwa wachezaji siku mbili kabla ya mechi na hizo taarifa za Sh250 milioni hana taarifa nazo kwa sasa.