Dakika 90 nyingine ngumu Yanga

Arusha. Yanga baada ya kipigo cha kwanza msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara, leo inarudi uwanjani tena ikiwa ugenini na safari hii ikiwa na vita na timu ya Polisi Tanzania katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa.

Timu hiyo itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi yake ya 22 msimu huu dhidi ya Coastal Union wiki hii ilipofungwa mabao 2-1 mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Matokeo ya mchezo huo bahati mbaya Yanga haina wa kumlaumu zaidi ya kujilaumu kwa kupoteza nafasi nyingi za wazi na hapo ndipo inapotakiwa kubadilika kuelekea mchezo wa leo.

Lengo la Yanga katika kutafuta ushindi halitakuwa rahisi kutimia kutokana na rekodi ya wenyeji wao wawapo nyumbani, ambapo msimu uliopita almanusura ilale baada ya kulazimisha sare.

Kikosi hicho cha kocha Cedric Kaze huenda kikawa na mabadiliko machache ambapo eneo ambalo huenda likabadilika zaidi ni safu ya ushambuliaji na hata viungo washambuliaji.

Bado hakuna uhakika kama mshambuliaji Michael Sarpong atakuwa tayari kwa mchezo huo uwezekano ukipungua kutokana na kuumia katika mchezo uliopita.
Hata hivyo, Yanga itashusha presha kutokana na kurejea kwa Yacouba Sogne ambaye katika mchezo dhidi ya Coastal Union aliingia kipindi cha pili.

Mbali na Sarpong, mabadiliko mengine yanaweza kumshuhudia winga Farid Mussa akirudi benchi kutokana na kuingia lawamani katika mchezo uliopita alioonyesha kiwango cha chini, ilhali Deus Kaseke anaweza kuanza ambapo itakumbukwa kiungo huyo alikuwa na kiwango bora anapocheza na Sogne - wakitengeneza ‘kombinesheni’ nzuri baina yao.
Yanga ambayo tangu juzi ilipofika mjini hapa imekuwa na vikao vya ndani kati ya viongozi na makocha, kisha mabosi na wachezaji wakipanga mkakati wa kupata matokeo mzuri ambayo kama yasipopatikana yanaweza kuondoa ndoto zao za kuchukua mataji mawili msimu huu.

Kiungo wa timu hiyo, Mukoko Tonombe ambaye ni nahodha wa tatu aliliambia gazeti hili kuwa hakuna anayetakiwa kubadilika zaidi ya wao wachezaji kama wanataka ushindi katika mchezo wa leo.

Mukoko alisema maombi yake ni kumuombea kila atakayepata nafasi ya kucheza kikosini kuitumia vyema jambo ambalo litawapunguzia presha wachezaji.
“Tumewaangusha sana mashabiki wetu, nikiwaona wanaolia inaumiza, lakini ni sisi wachezaji wa kubadilisha hili, ninachozidisha kuomba ni kila atakayepata nafasi aweze kutulia na kufunga,” alisema Mukoko.

“Tunapoteza nafasi sana kama tukifunga mabao ya kutosha itawarudishia ari ya kujiamini mabeki na hata sisi viungo, bado tuna nafasi ya kubadilisha mambo.”

Polisi ambao wataingia katika mchezo huo wakiwa na morali baada ya kushinda mechi iliyopita dhidi ya KMC hawatataka kufanya kosa kama walivyofanya msimu uliopita au walipofungwa katika mzunguko wa kwanza.

Kocha wa Polisi Tanzania, Malale Hamsini alisema anatarajia mchezo huo kuwa mgumu kutokana na jinsi wapinzani wao walivyo na presha ya matokeo baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union.

“Tuko vizuri na tayari kwa ajili ya mchezo, lakini najua kuwa utakuwa mgumu kwa sababu Yanga wametoka kupoteza, hivyo lazima watatukabili wakitaka kumaliza hasira zote kwetu, ila niwaambie tu hata sisi tumejipanga kwa sababu tunahitaji pointi tatu zitakazotuweka mahali pazuri kwenye msimamo wa ligi ,” alisema kocha huyo.

Malale alisema katika mchezo huo atamkosa kiungo wake, Abdulaziz Makame ambaye amezuiwa na Yanga kucheza mchezo huo kwani ni mchezaji wao na alipeleka kwa mkopo katika timu hiyo.

Mbali na mchezo huo, Wagosi wa Kaya ‘Coastal Union’ watawaalika KMC katika Uwanja wa Mkwakwani, huku Mtibwa wakitarajia kuwa wenyeji wa Gwambina FC mchezo utakaopigwa Jamhuri mjini Morogoro.