Doumbia apangua beki, kiungo Yanga

Dar es Salaam. Beki wa Yanga, Mamadou Doumbia raia wa Mali, ameanza kazi ya kuitumikia timu hiyo kuanzia juzi, huku akionyesha maufundi ambayo huenda yakamfanya kocha wa timu hiyo, Nassredine Nabi kupangua safu yake ya ulinzi na kiungo.

Doumbia anayecheza eneo la beki wa kati, ataleta mabadiliko makubwa kwa Yanga na si kwenye safu ya beki tu, bali hadi ya kwenye eneo la kiungo, ambalo ndiyo mhilili mkubwa wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu na Kombe la ASFC.

Msimu huu, Yanga imekuwa ikiwatumia Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Yanick Bangala na Mohamed Ibrahim ‘Bacca’ katika eneo la ulinzi wa kati, lakini ujio wa Doumbias huenda ukabadilisha kila kitu.

Beki huyo anatarajiwa kucheza na mmoja kati ya Job, Mwamnyeto, Bacca na Bangala, hivyo kuna ambao watakaa bechi wakisikilizia, kabla ya kuguswa eneo la kiungo.

Lakini pia, ujio wa Doumbia huenda ukapangua eneo la kiungo wa chini, msimu huu wamecheza sana Kharid Aucho, Salum Abubakar ‘Sureboy’, Zawadi Mauya na Mudathir Yahya aliyesajiliwa dirisha dogo na kuanza kwa kasi.

Kuna uwezekana mkubwa Bangala akarudi kwenye eneo la kiungo mkabaji, ambalo alicheza kwa kiwango bora msimu uliopita pamoja na Aucho na kuibuka mchezaji bora wa ligi na ikiwa hivyo kutakuwa na ushindani mkubwa wa namba kati yake, Mauya, Aucho, Sureboy na Mudathir.

Hata hivyo, kocha Nabi aliliambia gazeti hili kuwa anahitaji beki wa kati mwenye ubora wa hali ya juu ili aweze kumrudisha Bangala kwenye kiungo na Doumbia huenda akatimiza hitaji hilo.

Mwamnyeto, ambaye alitoka kikosini kutokana na Bangala kurudishwa nafasi ya beki wa kati akicheza na Job kwenye michezo ya hivi karibuni, ameonyesha kuwa bora akicheza sambamba na Job baada ya kukosekana kwa Bangala.

Pia Yanga ina mashindano mengi inashiriki huenda kila mchezaji akapata nafasi ya kucheza kulingana na uhitaji kwani inaiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi Kuu Bara.

Job alisema hana hofu na ujio wa Doumbia, kwani hata alipokuwa anajiunga na timu hiyo aliikuta ikiwa na mabeki wenye ubora na kutishwa kuwa hawezi kupata nafasi, lakini ni mchezaji ambaye amecheza michezo mingi zaidi ya wengine.