Kaseke aanika nondo

DEUS Kaseke amejua kuwapa raha mashabiki wa Yanga msimu huu, kwa mabao aliyofunga na kuipa timu yao pointi muhimu, lakini nyuma ya makali hayo kwa msimu huu, winga huyo amefichua kilichobeba akisema Mungu amekuwa na upande wake na kumuepushia magonjwa.

Kaseke alisema kuzingatia miiko ya soka, ikiwemo nidhamu, bidii na uvumilivu ni wajibu wa kila mchezaji aliye na malengo ya kufika mbali, lakini kama Mungu hajamjalia afya njema inakuwa kazi bure na hawezi kufika popote kwenye kazi yake hiyo.

Kwenye msimamo wa wafungaji wa Yanga, anayeongoza kwa mabao ni Yacouba Sogne (saba) na Kaseke anashika nafasi ya pili akiwa na (sita na asisti tano), jambo ambalo alisisitiza kwamba bila uvumilivu wa kistahimili changamoto za hapa na pale ni ngumu kufanya vizuri.

“Kazi ya soka inahitaji moyo wa ustahimilivu ili kuweza kuzikabili changamoto mbalimbali kwani hakuna kazi ambayo inakosa mitihani, ndio maana nimesema Mungu msimu huu alikuwa upande wangu mimi huduma yangu kuwa na kibali,” alisema Kaseke na kuongeza;

“Kikubwa sipendi kuangalia vikwazo, bali napigania sana ni namna gani natakiwa kuzitumiza ndoto zangu kwa kipindi hiki ambacho nina wakati mzuri wa kucheza, kwani kila zana na zana zake, ndio maana walikuwepo waliowika na wamepumzika wanafanya shuguli nyingine.”

Kaseke alisema pamoja na bidii anayoifanya ya kuzingatia mazoezi ya timu na yaike binafsi, bila ushirikiano na wachezaji wenzake anatambua asingeweza kufanikisha mabao sita aliyofunga.

“Ukiona mchezaji anafanya vizuri kuna wachezaji wenzake ambao wamefanikisha kiwango chake kuwa bora na ndio maana uwanjani tupo wachezaji 11,” alisema.