Mashabiki Man City, Spurs kupimwa corona mara tatu

Wednesday April 14 2021
corona pic
By AFP

Mashabiki watakaotaka kuingia uwanjani kuona mechi ya fainali ya Kombe la Ligi Aprili 25 kati ya Manchester City na Tottenham, watatakiwa wawe na uthibitisho kuwa wamepima na kugundulika hawana maambukizi ya virusi vya corona ndani ya saa 24 kabla ya mechi.


City na Tottenham zitapewa tiketi 2,000 kila moja kwa ajili ya mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Wembley, mchezo utakaotumiwa kama jaribio kupima mashabiki kabla ya kuingia viwanjani.


Jumla ya mashabiki 8,000 wataruhusiwa kuingia uwanjani kuona mechi hiyo, huku asilimia 50 ya tiketi nyingine ikienda kwa wakazi wa maeneo ya karibu na Wembley na wafanyakazi wa Huduma ya Taifa ya Afya.


Ili kuingia uwanja wa Wembley, mashabiki watalazimika kufanya kipimo cha corona katika maeneo yaliyotengwa ndani ya saa 24 kabla ya mchezo na kuonyesha uthibitisho kuwa hawana maambukizi.


Pia watatakiwa kufanya vipimo vya PCR nyumbani. Kimoja kabla ya kusafiri kuelekea uwanjani na kingine siku tano baadaye.


Hata hivyo, uamuzi wa kutoruhusu mashabiki wowote wenye umri chini ya miaka 18 kuhudhuria na kuwaambia watu ambao wako katika hali ambayo si nzuri kiafya au wajawazito, wasiombe kuuziwa tiketi, umeelezewa na kundi la watu wenye ulemavu la Tottenham kuwa ni ubaguzi.

Advertisement


Kundi hilo, SpursAbility limesema katika taarifa yake: "Uamuzi uliochukuliwa kwa ajili ya mechi hii ni ubaguzi wa moja kwa moja kwa mashabiki wengi wenye ulemavu.


"Baadhi ya mashabiki wetu wamejikinga kwa zaidi ya miezi 12 na waliiona mechi hii kama fursa ya kurejea katika baadhi ya aina ya maisha ya kawaida.


"Mechi inaruhusu watazamaji 8,000 tu ndani ya uwanja wenye uwezo wa kuchukua watu 90,000 - chini ya asilimia tisa. Bado kuna uamuzi wa kutoruhusu kundi dogo la mashabiki ambao watahitaji kutoa taarifa zao kwa hiari."

Advertisement