Mfaransa wa Yanga awawahi Biashara fasta Dar

YANGA wanafanya kila linalowezekana Kocha wao mpya, Sebastian Migne awawahi Biashara Jijini Dar es Salaam wikiendi hii.

Vigogo wa Yanga baada ya sare ya bao 1-1 na KMC walikutana Jijini Dar es Salaam pamoja na wachezaji na benchi la ufundi na baada ya kikao hicho wakakubaliana kwamba Migne aje mapema ili kuamsha morali ya wachezaji zaidi.

Mwanaspoti linafahamu kwamba mabosi wa juu wa Yanga baada ya kuziona dakika 90 ngumu dhidi ya KMC, walikutana na wachezaji ambapo waliwaambia hata wao hawaelewi kilichotokea. Mmoja wa vigogo wa Yanga kwenye kikao hicho aliiambia Mwanaspoti kwamba Saido Ntibazonkiza aliwaambia kwamba hajawahi kukosa nafasi nyingi kama zile tangu aanze kucheza Jangwani.

Viongozi wa Yanga wanaamini kwamba ujio wa Migne licha ya kwamba wanafanya siri jina lake lakini utaibua morali haswa kwenye Kombe la FA.

Mwenyekiti wa Kamati ya ufundi ya klabu hiyo, Dominic Albinius ameliambia Mwanaspoti kwamba ndani ya siku chache kutoka sasa watakuwa wamemleta kocha huyo huku akigoma kuthibitisha kwamba ni Migne au kuna mwingine ingawa Mwanaspoti lina uhakika asilimia zote.

“Siwezi kukwambia ni nani tunamleta klabu itamtangaza lakini tumeona sasa ni haraka tunahitaji kocha ambaye atakuja kusaidiana na Juma Mwambusi.

“Kuna mambo ambayo tumeyabaini na tumelazimika tuchukue hatua hiyo ya haraka katika kuinusuru timu, tumekuwa na vikao na wachezaji lakini hata makocha na benchi lao yapo ambayo tumeona tuyafanyie kazi kwasasa na mengine baadaye,” alisema.

Aliongeza kuwa ujio wa Migne unaweza kuwa na tija kwa wachezaji wao ama kilio kwamba atapewa kazi ya kufanya tathimini ya mchezaji gani anataka kuendelea naye au kuwaondoa kulingana na viwango atakavyoona.

Alisema uamuzi huo unalenga kutaka kuona msimu ujao wanakuwa na timu bora ya ushindani ambayo itatokana na uamuzi wa Mfaransa huyo.

“Lengo letu tunataka aione timu kwa macho yake na ndio maana tunataka aje mapema wakati huu inacheza hapa nyumbani ili ajue ubora wa wachezaji lakini awe na uwezo wa kuamua juu ya baadhi ya wachezaji.

“Tunataka kumpa nafasi ya kusajili timu kwa akili yake na hatua hiyo tunataka ianze kwa kuangalia ubora wa wachezaji tulionao halafu aseme anataka nini ili ligi ikiisha tumletee mchezaji anayemtaka atupe matokeo.

“Kuna uwezekano mkubwa tukawaondoa baadhi ya wachezaji na narudia vigezo ni vilevile ubora kwa maana ya viwango lakini kuna suala la nidhamu pia litahusika,”alisema. Migne licha ya kwamba hajafundisha klabu kubwa za Afrika lakini ameifikisha Kenya kwenye Afcon.