Mfumuko wa bei wabakia kama Septemba

Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Makazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Ruth Minja.

Muktasari:

Mfumuko huo kwa mwaka ulioishia  Oktoba  umebaki kuwa asilimia 3.1 kama ilivyokuwa  Septemba.

 

Dodoma. Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema kubakia kwa mfumuko wa bei kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioshia Septemba 2020, kumechangiwa na kupungua pamoja na kuongezeka kwa bei ya bidhaa mbalimbali ukilinganisha na mwaka ulioshia Oktoba 2020.

Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Makazi wa NBS Ruth Minja amesema leo Novemba 9, 2020, kuwa mfumuko huo wa bei umebaki kuwa asilimia 3.1 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioshia Septemba 2020.

Amezitaja baadhi ya bidhaa za vyakula zilizopungua bei kwa Oktoba 2020 ukilinganisha na Oktoba 2019 ni mchele kwa asilimia 4.2, mahindi kwa asilimia 12.4, unga wa ngano kwa asilimia 0.9 na  unga wa mtama kwa asilimia 0.8.

Nyingine zilizopungua bei ni  ni unga wa muhogo kwa asilimia 14, mihogo mibichi kwa asilimia 2.5, viazi vitamu kwa asilimia 5.4 na ndizi za kupikia kwa asilimia 6.3.

Kwa upande mwingine Ruth ametaja baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizilizoongezeka bei ni kwa Oktoba 2020 zikilinganishwa na Oktoba 2019 ni pamoja na mavazi kwa asilimia 2.2 na gesi ya kupikia kwa asilimia 6.5.

Bidhaa nyingine zilizoongezeka bei ni mkaa kwa asilimia 8.8, ukarabati wa vifaa vya usafiri kama magari kwa asilimia 8.3 na samani kwa asilimia 1.4.