Mgunda atoa mwelekeo Simba

BAADA ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye mzunguko wa kwanza, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda, amesema wanatakiwa kufanya kazi kubwa katika mzunguko wa pili ili kutimiza malengo yao baada ya Yanga kukaa kwenye nafasi yao kwa sasa.

Simba imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa imepoteza mchezo mmoja na kutoka sare mara nne ikiwa nafasi ya tatu na pointi 34.

Hata hivyo, takwimu kabla ya mchezo wa jana kati ya Yanga na Namungo zilionyesha Simba ndiyo timu pekee ambayo imefunga mabao mengi kwenye ligi ikifunga mabao 31 na ikiwa imeruhusu mabao saba tu.

Mgunda alisema malengo yao yalikuwa ni kumaliza mzunguko wa kwanza kwa kuongoza ligi lakini hilo limeshindikana baada ya Yanga kuwapiga bao na kuaangukia nafasi ya tatu bila kutarajia.

“Tumeshindwa kufikia lengo tutarudi kwa kasi mzunguko wa pili ili kufikia malengo ya kutwaa ubingwa msimu huu, tumewasoma wapinzani wetu wote mzunguko wa kwanza, tumeona tulipoteleza sasa ni jukumu la kusawazisha makosa,” alisema Mgunda.