Mkwassa afungukia ishu ya kujiuzulu Ruvu

KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa amesema wakati wowote atawasilisha barua kwa uongozi ili kujiuzulu nafasi hiyo kutokana na matokeo mabaya ya kikosi hicho.

Mkwasa ambaye amekuwa akiinoa timu hiyo mara kwa mara aliliambia gazeti hili kuwa kutokana na anavyoipenda na kuiheshimu Ruvu Shooting anaona bora akae pembeni kulinda heshima ya klabu hiyo na yake pia.

Tangu ilipopata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union katika mchezo uliofanyika Septemba 29, mwaka huu, Ruvu Shooting haijaonja tena ushindi katika michezo yake 10 iliyopita.

Katika michezo hiyo 10, imepoteza minane na kutoka sare miwili huku ikidaiwa kushuka ubora kwa timu hiyo kumechangiwa na kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wake waliokwenda katika kozi za kijeshi.

Hali hiyo ndio imesababisha Mkwasa kutaka kuchukua uamuzi huo mgumu.“Kutokana na mwenendo wa timu nimeona ni heri nikae pembeni kwa kuwa Ruvu ni klabu yangu na naipenda na naiheshimu, hivyo nimeona mambo yasiwe mengi kwa kulinda heshima yangu na klabu pia.

“Nimeshaongea na wachezaji wangu kuwaambia jambo hilo na nataka kuwasilisha barua rasmi ya uamuzi wangu kwa uongozi wa timu muda wowote kuanzia leo (jana),” alisema Mkwasa.

Kama Mkwasa atajiuzulu atakuwa kocha wa sita kutomaliza msimu na timu baada ya Mserbia Zoran Maki wa Simba naye kuvunjiwa mkataba Septemba mwaka huu, Mrundi Masoud Djuma wa Dodoma Jiji kutimuliwa kama ilivyo kwa Mkenya, Francis Baraza wa Kagera Sugar.

Wengine ni Mrundi Joslin Bipfubusa wa Polisi Tanzania na Mfaransa Denis Lavagne wa Azam.