Mwakinyo apewa ulaji

Muktasari:

Hii ni mara ya saba kwa rais huyo wa WBF, Goldberg Howard kuwasili nchini kwa shughuli za masumbwi nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Rais wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa la Dunia (WBF), Goldberg Howard amesema kama bondia Hassan Mwakinyo atatetea ubingwa wa Shirikisho hilo wa mabara kesho, atakidhi viwango vya kuwania ubingwa wa dunia.

Howard ametamka hayo jana alipowasili nchini sanjari na mwamuzi wa kimataifa, Edward Marshal kutoka Afrika Kusini ili kusimamia pambano la Mwakinyo na Jose Carlos Paz wa Argentina litakalopigwa kwenye Ukumbi wa Next Door Arena, Dar es Salaam.

Mwakinyo atapanda ulingoni kutetea ubingwa wa mabara wa WBF kwenye uzani wa super welter, pambano la raundi 10 likalochezeshwa na Marshal na kusimamiwa na Howard sanjari na viongozi wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC).

Akizungumza baada ya kuwasili nchini akiwa na mkanda ambao Mwakinyo na Paz watagombea, Howard alisema kama Mtanzania huyo atashinda, itakuwa ni fursa kwake kuwania mkanda wa dunia Februari mwakani.

“Atacheza na bondia kutoka Georgia, Lasha Gurguliani, lakini kama atautetea ubingwa wake wa mabara kesho, kinyume na hapo hawezi kupata nafasi hiyo,” alisisitiza Howard, ambaye amewasili nchini na vifaa ikiwamo glovu mpya ambazo ndizo Paz na Mwakinyo watavitumia ulingoni.

Howard pia amewapongeza waandaaji, kampuni ya Jackson Group Sports kwa kutimiza sheria na kanuni zote za WBF kuandaa pambano hilo la ubingwa linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa ndondi nchini.

Aidha, Mwakinyo na Paz watakutana kwa mara ya pili katika zoezi la kupima uzito na afya leo, ikiwa ni baada ya juzi kukutana uso kwa uso ‘face off’, kila mmoja akijinasibu kuondoka na ubingwa kesho.

Mwakinyo alimwambia mpinzani wake kuwa anataka kumuonyesha tofauti kati ya bondia na bondia profesheno, akisisitiza kwa maandalizi aliyoyafanya kambini kwake Tanga, mpinzani wake hatoki.

Paz alijibu tambo hizo akidai amekuja Tanzania kuchukua mkanda huo, hivyo Mwakinyo, ambaye anautetea aubebe kwa mara ya mwisho mwisho kwani kesho jioni ndiyo itakuwa mwisho wa bondia huyo namba moja nchini kuumiliki.

Mkurugenzi wa Jackson Group Sports, Kelvin Twissa alisema maandalizi ya pambano hilo yamekamilika na mbali na Marshal na Howard, mabondia wa Zambia, Zimbabwe na DR Congo ambao pia watazichapa kusindikiza ubingwa wa Mwakinyo na Paz wamewasili.

Mabondia hao ni Alice Mbewe wa Zambia atakayecheza na Zulfa Macho, Alex Kabangu wa DR Congo atakayezichapa na Hussein Itaba, Fatuma Zarika wa Kenya atakayecheza na Patience Mastara wa Zimbabwe.

Tayari tiketi za pambano zimeanza kuuzwa kwa njia ya selcom kwa Sh3 milioni kwa meza ya watu 10 na Sh150,000 kwa viti vya kawaida.