Phiri aomba wiki mbili za kibabe Msimbazi

Phiri: Makombe yanakuja, atoa ramani ya kubeba CAF

STRAIKA mpya wa Simba, Mzambia Moses Phiri amewaambia viongozi wa timu hiyo kwamba ; “Nipeni wiki mbili tu.”

Staa huyo aliyemalizana na Simba juzi Jijini Dar es Salaam, anaondoka nchini leo kurejea kwao tayari kujiweka sawa kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa inayoanza Agosti 12 mwaka huu.

Akizungumza na Mwanaspoti jana jijini Dar es Salaam, Phiri alisema; “Nimeomba wiki mbili nikaweke mambo yangu sawa na nikirudi ni kazi tu.”

“Nikirudi ni kupitiliza kambini tu maana muda huo tayari nadhani kambi ya msimu mpya itakuwa imeanza, nadhani kila kitu kitakuwa sawa, nimepania sana kuanza kazi na Simba na natarajia ushirikiano utakuwa wa hali ya juu,”alisema mchezaji huyo ambaye Mwanaspoti linajua jana aliachwa na ndege kutokana na adha za foleni za Dar es Salaam.

Phiri ambaye anasifika kwa uzoefu wake kimataifa pamoja na usumbufu wake mbele ya lango, amejiunga na Simba inayosaka Kocha Mkuu, akitokea Zanaco ya Zambia ambapo kabla ya kusaini Msimbazi alikuwa akiwindwa na klabu kadhaa Yanga ikiwemo.

Amesaini miaka miwili Simba akisema kilichomsukuma ni mpangilio mzuri aliouona kuanzia kwenye uongozi mpaka jinsi wachezaji wanavyoishi na hata Wazambia wenzie, Clatous Chama na Larry Bwalya aliyeagwa jana Simba.

“Kitu cha muhimu sana ni kushinda vikombe nba kuisaidia timu. Nikipata ushirikiano mzuri nitafanya kazi kubwa,naahidi tutarudi kwenye kasi yetu ya kushinda vikombe,” alisema Phiri ambaye amewaahidi mashabiki kwamba kama akipata ushirikiano mzuri kutoka kwa wenzake anaamini kwamba kila kitu kitakwenda sawa na Simba ina uwezo wa kucheza hata fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba iko kwenye harakati za kusuka upya kikosi chake ikiingiza sura kadhaa mpya ambazo zitawasaidia kurejesha mataji waliyoyapoteza msimu huu likiwemo lile la Ligi Kuu Bara na Kombe la FA. Kwa mujibu wa uongozi wa Simba lengo kubwa na namba moja la msimu ujao ni kucheza nusufainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwani hatua ya robofainali wamecheza sana. Muda wowote kuanzia leo Simba inaweza kutangaza Kocha mpya mbadala wa Pablo Franco aliyetimuliwa hivikaribuni baada ya kushindwa kufikia malengo ya mkataba wake.