Pitso: Yanga ina majembe

Pitso: Yanga ina majembe

MASHABIKI wa Simba huko mtaani wanachekelea sana Yanga kufungwa mabao 2-0 na Vipers ya Uganda katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kwenye tamasha la Wiki ya Mwananchi lililofanyika juzi, lakini Kocha Msauzi Pitso Mosimane aliyekuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa amefichua jambo.

Kocha huyo aliyeondoka jana Jumapili usiku kurudi Sauzi baada ya kualikwa na Yanga kwenye tamasha hilo, alisema mabingwa hao wa nchi wana kikosi chenye wachezaji wenye vipaji vikubwa lakini wachezaji hao wanahitaji muda kidogo wa kupiga mazoezi makali ili kuwasha moto kwenye michuano watakayoshiriki.

Pitso aliyekuwa nchini kwa mwaliko wa siku tatu na aliyeendesha kliniki maalumu ya soka la vijana, alisema ameiangalia Yanga ikivaana na Vipers na kukikiri ina timu bora ambayo hata hivyo inahitaji muda kidogo iweze kupewa mazoezi ya kutosha.

Alifafanua kazi ya Yanga kuonyesha ubora huo itabaki kwa wachezaji ambao wakitulia na kuwasikiliza makocha wao watatisha, kwani wana vipaji na uwezo wa hali ya juu uwanjani.

“Hii timu nimeambiwa ilimaliza msimu bila kupoteza, nimewaona wachezaji ni bora lakini wanahitaji muda kidogo kuweza kuandaliwa kwa makali zaidi,” alisema Pitso alipozungumza na Mwanaspoti mapema jana.

“Nilichokiona licha ya kuwa na vipaji na uwezo, lakini wachezaji walikuwa wanacheza kawaida sana ni sahihi nikisema walikuwa wanasherehekea siku yao na mashabiki wao, lakini kocha atajua wapi pa kuanzia.”

Kocha huyo aliyetwaa ubingwa wa Afrika akiwa na klabu za Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Al Ahly, alisema ameambiwa Yanga itakuwa na mchezo mgumu dhidi ya Simba wa Ngao ya Jamii wikiendi hii, hivyo anaamini matokeo ya Vipers yatamsaidia Kocha Nasreddine Nabi.

“Unapokwenda kucheza mechi ngumu dhidi ya wapinzani wenu kama kocha ukipata matokeo kama haya kabla yanakusaidia, unajua kila utakachokisisitiza kwa wachezaji wako watakuwa makini, haya matokeo yatawasaidia kuamka kwa nguvu kwenye maandalizi yao,” alisema.

Katika mechi hiyo ya pili kwa Yanga kupoteza siku ya Tamasha lao tangu liliasisiwe mwaka 2009, wageni walipata mabao katika kila kipindi, yakiwekwa kimiani na Milton Karisa na Bright Anukani.