PSG yaivua ubingwa Bayern ikikubali kipigo finyu

PSG yaivua ubingwa Bayern ikikubali kipigo finyu

Muktasari:

  • Kwa miaka kumi iliyopita, uhusiano wa Paris Saint-Germain na Ligi ya Mabingwa wa Ulaya umezongwa na fadhaha pamoja na vipigo, lakini matokeo ya jumla yaliyowavua ubingwa Bayern Munich, ni makubwa tangu matajiri wa Qatar waichukue klabu hiyo ambayo ina hamu ya kuonja ubingwa wa soka Ulaya.

Paris, Ufaransa (AFP). Kwa miaka kumi iliyopita, uhusiano wa Paris Saint-Germain na Ligi ya Mabingwa wa Ulaya umezongwa na fadhaha pamoja na vipigo, lakini matokeo ya jumla yaliyowavua ubingwa Bayern Munich, ni makubwa tangu matajiri wa Qatar waichukue klabu hiyo ambayo ina hamu ya kuonja ubingwa wa soka Ulaya.


Dhidi ya timu ambayo kocha Mauricio Pochettino amekuwa akisisitiza kuwa ndiyo bora barani Ulaya, PSG ililipiza kisasi cha kufungwa bao 1-0 na Wajerumani hao katika fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.


Lakini haikufanikiwa kulipa kisasi bila ya kuumizwa; ilifungwa bao 1-0 nyumbani jana Jumanne usiku, lakini ushindi mkubwa wa mabao 3-2 ilioupata katika mechi ya kwanza jijini Munich ulitosha kuipeleka PSG nusu fainali.


Bao pekee la jana lilifungwa na Eric Maxim Choupo-Moting, akiizamisha timu yake ya zamani.


Kwa kuangalia mchezo wa jana kulinganisha na miaka iliyopita, PSG ingeweza kuchanganyikiwa baada ya kuwekwa katika presha kubwa, lakini safari hii ilitulia na kuhimili mikiki na hatimaye kupata ushindi huo wa sheria ya bao la ugenini baada ya matokeo kuwa 3-3 na hivyo kutangulia nusu fainali kuisubiri Manchester City au Borussia Dortmund zinazocheza leo usiku.


Baada ya kampuni ya Qatar Sports Investments kuichukua mwaka 2011, PSG imetumia muda mrefu kutafuta mafanikio katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa.


Ilipoteza uongozi wao wa mechi ya kwanza na kuondolewa kwa sheria ya bao la ugenini na  Chelsea katika robo fainali za mwaka 2014 na baadaye mbele ya Manchester United katika hatua ya 16 bora mwaka 2019.


Pia kulikuwa na kipigo cha fedheha mwaka 2017 wakati ushindi wa PSG mabao 4-0 katika mechi ya kwanza ya hatua ya 16 bora, ulifutwa na kipigo cha mabao 6-1 ilichopewa na Barcelona katika mechi ya marudiano.


Safari hii waliweza kulinda ushindi wao licha ya nahodha Marquinhos na kiungo Marco Verratti kukosa mechi hiyo ya marudiano na Neymar kupoteza nafasi kadhaa katika kipindi cha kwanza.


"Klabu hii imekuwa ikikua kila siku, mwaka kwa mwaka," alisema Presnel Kimpembe, nahodha wa mechi dhidi ya Bayern na ambaye mpira aliounawa miaka miwili iliyopita ulisababisha timu hiyo itolewa na Manchester United.

Hakuna kisingizio kwa Neymar, Mbappe
Mafanikio ya jana dhidi ya mabingwa watetezi yamekuja baada ya PSG kuiondoa Barcelona katika hatua ya 16 bora, ikishinda kwa mabao 4-1 kwenye uwanja wa Camp Nou katika mechi ya kwanza.


Ushindi huo pia ulikuwa ni wa kisasi dhidi ya Barcelona ambayo iliishinda PSG mara tatu katika hatua za mtoano za muongo uliopita.


Katika mechi hizo zote, PSG imeonyesha uthabiti ambao umekuwa ukikosekana na wamewaondoa wapinzani wawili wakubwa miongoni mwa vigogo wa Ulaya wakati wakielekea nusu fainali, baada ya kuwafunga Manchester United ugenini katika hatua ya makundi.


"Tunastahili kushinda mechi hizi mbili, lakini sidhani kama hilo linatufanya tupewe nafasi ya kuwa bingwa," alisema kocha Pochettino na bado safari hii ushindi wao umekuwa dhidi ya vigogo.


Mwaka jana, safari yao kwenda fainali, ilihusisha ushindi dhidi ya Dortmund, Atalanta na RB Leipzig, ambazo hazikuwa zikipewa nafasi ya kutwaa kombe. Ushindi katika hatua mbili za mwisho ulikuwa katika mechi mojamoja za kuanzia hatua ya robo fainali zilizochezwa Lisbon.


Mwenendo wa PSG barani Ulaya msimu huu umekuja wakati ubabe wao nyumbani ukiwa shakani -- baada ya kutwaa mataji saba katika miaka nane--, kwa sasa inashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Ufaransa ikizidiwa kwa tofauti ya pointi tatu na Lille, huku zikiwa zimesalia mechi sita.


Pamoja na yote, kombe la Ligi ya Mabingwa ndicho kitu kikubwa na ni mafanikio hayo katika michuano hiyo mikubwa ya Ulaya ndiyo yanayoweza kuwashawishi nyota wawili, Kylian Mbappe na Neymar kuongeza mikataba yao.


Mikataba ya wachezaji hao ghali wawili katika historia ya soka wakati walipowasili Paris mwaka 2017, inaisha mwishoni mwa msimu ujao. Ndoto ya Barcelona inaendelea kuwa ni kumrejesha Neymar, wakati kwa muda mrefu Mbappe amekuwa akihusishwa na Real Madrid.


"Kylian na Neymar hawana kisingizio cha kuondoka kwa sababu tuna kila kitu cha kutuwezesha kutwaa kombe la Ligi ya Mabingwa," rais wa PSG, Nasser al-Khelaifi aliiambia RMC Sport.
"Kwa sasa timu yetu ni kubwa, kwa kujali pia timu nyingine zote."