Sakho, Banda waletewa fundi mpya Simba

Muktasari:

  • Taarifa kutoka ndani zinaeleza mabosi wa Simba wameanza harakati za kuboresha benchi la ufundi na kulipa nguvu za wataalamu wapya pamoja na kuwafuatilia wachezaji wapya ambao watawasajili kwenye dirisha dogo akiwemo straika Mghana Kwame Opoku.

DILI linanukia. Simba itamtambulisha kocha mpya viungo aliyekuwa akifundisha kwenye nchi za Kiarabu na kabla ya wiki hii kumalizika.

Taarifa kutoka ndani zinaeleza mabosi wa Simba wameanza harakati za kuboresha benchi la ufundi na kulipa nguvu za wataalamu wapya pamoja na kuwafuatilia wachezaji wapya ambao watawasajili kwenye dirisha dogo akiwemo straika Mghana Kwame Opoku.

Maboresho ya kwanza kuna mtaalamu ‘fundi’ na kocha wa viungo aliyekuwa akifundisha kwenye nchi za Kiarabu kuja kukabili tatuzo la wachezaji kuumia mara kwa mara akiwamo Pape Ousane Sakho na Peter Banda walioumia wiki iliyopita.

Mtaalamu huyo anakuja kuchukua nafasi ya Karim Sbai aliyeondoka pamoja na kocha, Zoran Maki.

Inaelezwa mtaalamu wa kuchua misuli ndani ya Simba, Msauzi Fareed Casssiem ndio amempendekeza kocha huyo wa viungo na kuwahakikishia mabosi zake pamoja na kocha mkuu, Juma Mgunda atakuja kuongeza nguvu kulingana na mahitaji ya msingi ndani ya timu wakati huu.

Maboresho ya pili Simba haina kocha wa makipa tangu alivyoondoka Mmorocco Mohamed Rachid aliyekuwa akifanya kazi kwa pamoja na Zoran aliyetimkia Misri.

Kama umefuatilia mechi mbili za Simba dhidi ya Singida Big Stars na Ihefu wakati wa kupasha misuli moto makipa, Aishi Manula na Benno Kakolanya walikuwa wanafanyishwa mazoezi na mwenzao chaguo la tatu, Ally Salim aliyekuwa anafanya majukumu ya kocha wa makipa.

Kikosi cha Simba kabla ya kucheza mechi na Ruvu Shooting Novemba 19, kitakuwa tayari kimemtambulisha kocha mpya wa makipa na wakati huo atakuwa ameanza kazi ya kuwanoa, Manula, Kakolanya na Salim.

Baada ya maboresho hayo mawili mabosi wa Simba watafanya kikao kingine kizito cha uamuzi wakati kocha, Selemani Matola yupo kwenye masomo ya ukocha wa leseni ‘A’ ya CAF katika timu Mgunda atabaki mwenyewe au watatafuta kocha mwingine wa kusaidiana naye.

Alipotafutwa Mgunda alisema suala la kuletewa kocha wa viungo hilo tayari amewasiliana na mabosi zake na wamemueleza siku si nyingi linakamilika.

Mgunda alisema si vyema kulizungumza wazi kwenye kila eneo ila kwake amelikamilisha na amewaambia viongozi aina ya kocha wa viungo anayemuhitaji ili kuja kuunganisha nguvu kwa pamoja.

“Kuhusu kocha wa makipa hilo nalo hivi karibuni linakwenda kukamilika kwani kuna ambao viongozi wanawafuatilia na naamini mmoja kati ya hao tunakwenda kumchukua,” alisema Mgunda na kuongeza;

“Tunafanya hayo yote kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye timu ili kufanya vizuri katika mashindano yote ndio maana tunaangalia hadi baadhi ya wachezaji wapya wa kuwasajili kwenye dirisha dogo ikiwemo straika mwenye uwezo wa kufunga.”