Simba yaonywa ukuta Klabu Bingwa

Muktasari:

Simba imetakiwa kuimarisha eneo la ulinzi kabla ya kuikabili Plateau United ya Nigeria katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa kati ya Novemba 27 hadi 29, mwaka huu.

Dar es Salaam. Simba imetakiwa kuimarisha eneo la ulinzi kabla ya kuikabili Plateau United ya Nigeria katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa kati ya Novemba 27 hadi 29, mwaka huu.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wamepangwa kuanzia ugenini hatua ya awali ya michuano hiyo kabla ya kucheza mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam kati ya Desemba 4 hadi 6.

Ikiwa Simba itavuka hatua hiyo itakutana na mshindi kati ya Costa do Sol ya Msumbiji na Platinum ya Zimbabwe.

Kufuatia kutolewa kwa ratiba ya mashindano hayo juzi na timu itakayokutana na Simba kufahamika, baadhi ya makocha nchini wameitahadharisha kutoibeza kutokana na kutokuwa maarufu kama zilivyo baadhi ya timu za Nigeria ikiwamo Enyimba.

Enyimba imekutana na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara mara kadhaa kwenye Ligi ya Mabingwa barani Afrika na kuwatoa katika hatua mbalimbali.

Kocha wa Biashara United, Francis Baraza ameitaka Simba kujipanga vizuri ili kuhakikisha kuwa inaichapa Plateau United ambayo inasifika kwa kutumia soka la nguvu.

Baraza alisema kipimo kizuri kama Simba iko tayari kwa ajili ya mashindano hayo makubwa barani humu ni kushughulikia tatizo la kiufundi lililoonekana ilipocheza na Yanga wiki iliyopita hasa eneo la ulinzi.

“Ile mechi dhidi ya Yanga ndio ilikuwa kipimo tosha cha utayari wa Simba kimataifa, lakini wameonekana kuwa wanapata shida wakikutana na timu inayotumia nguvu kubwa. Pia safu yao ya ulinzi bado ina tatizo wanatakiwa kujirekebisha haraka,” alisema.

“Kocha wao afanyie kazi eneo la ulinzi na jinsi wanavyoshambulia, pia iache kutegemea baadhi ya wachezaji mfano mkimbana Clatous Chama basi mmeipoteza Simba, timu inakuwa haisogei mbele kushambulia, sasa hilo jambo sio zuri wanapoelekea kwenye mashindano makubwa kama hayo.

“Safu ya ulinzi nayo ina makosa sana, hiyo ndio inatakiwa kujiangalia zaidi. Lakini pia timu nzima inatakiwa kuwasaidia mabeki, wasiwaachie peke yao kazi ya ulinzi kwani ulinzi unaanzia mbele.”

Baraza alisisitiza: “ Ni lazima wakabe kwa pamoja kama timu pindi wanapopoteza mpira, waache kuiga Yanga inavyofanya sasa wanapotafuta mpira unaona wanakwenda pamoja mpaka wanaupata.”

Naye kocha wa Mtibwa Sugar, Vincent Barnabas alisema upande wa ushambuliaji Simba haina tatizo kwani ina uwezo mkubwa wa kupata mabao katika mchezo huo, lakini inatakiwa kurekebisha udhaifu uliopo katika ulinzi.

“Simba udhaifu wao uko kwenye safu ya ulinzi hasa mabeki wa kati (Pascal Wawa na Joash Onyango) wanafanya sana makosa ambayo wasipoangalia yatawagharimu na ukizingatia hayo ni mashindano makubwa na unacheza mechi mbili tu unajua unasonga au unabaki, hivyo lazima wawe makini,” alisema.

Hata hivyo, Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema anaamini Simba itabadilika na kuingia kwenye mashindano hayo tofauti na inavyocheza katika Ligi Kuu.

“Naamini kabisa watafanya vizuri kwani wana wachezaji wazoefu ambao wameshiriki mashindano hayo msimu uliopita, hivyo sina mashaka nao licha ya kwamba watu wana hofu kutokana na kiwango walichoonyesha katika baadhi ya mechi kwenye ligi, sidhani kama wataenda hivyo kimataifa lazima wabadilike kulingana na mashindano yenyewe,” alisema Maxime.

“Muhimu ni kujipanga, kusahihisha kila kasoro katika kikosi kuanzia kipa mpaka kwenye safu ya ushambuliaji, kwani mpira hauwezi kufanya marekebisho eneo moja ndani ya kikosi kwa kuwa ili muwe bora ni lazima mcheze kama timu mkishirikiana kila eneo na hicho ndicho Simba wanatakiwa kukifanya.”

Wapinzani wa Simba

Plateau United ilianzishwa 1975 na inatumia Uwanja wa New Jos unaoingiza mashabiki 40,000.

Timu hiyo ilipata nafasi ya kuiwakilisha Nigeria kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya mlipuko wa corona uliosababisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Nigeria (NFF) kukatisha msimu wa ligi.

Hadi Ligi Kuu inasimama Plateau ilikuwa inaongoza kwa pointi 49 baada ya kucheza michezo 25, hivyo NFF iliipa nafasi hiyo wakati Enyimba itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Hofu ya kocha Plateau

Kocha wa Plateau United, Abdul Maikaba ameelezea hofu yake baada ya kupangiwa kuanza na Simba katika mashindano hayo.

Kocha huyo ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa wana kazi kubwa ya kufanya kabla ya kukabiliana na Simba.

Maikaba ameandika: “Simba wana kocha mzuri, wanacheza soka la kushambulia kwa nguvu, wanapenda kumiliki mpira na hupenda kuwanyima nafasi ya kucheza wapinzani wao. Hivyo kwa kuwa tunaujua udhaifu wetu tutahakikisha tunajiandaa na kuwa tayari kuwakabili.”

Enyimba kiboko ya Simba

Simba sio mara ya kwanza kukutana na timu za Nigeria kwani tangu 2005 imekutana na Enyimba ya huko mara tatu na zote ilipoteza.

Mwaka 2005 ilikutana nayo katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutupwa nje baada ya kipigo mabao 5-1. Ilianza na sare ya bao 1-1 Dar es Salaam kisha ikachapwa 4-0 huko Nigeria.

Kabla ya hapo, 2003 ilikutana na Enyimba katika makundi ya ligi hiyo ambapo ugenini ilifungwa mabao 3-0 na Dimba ilishinda Dar es Salaam kwa mabao 2-1.

Mwaka 2008 tena ilikutana na Enyimba katika hatua ya kwanza ya ligi hiyo na kutolewa kwa jumla cha mabao 7-1, ikianza kufungwa 4-0 ugenini na kisha nyumbani kwa mabao 3-1.