Taifa Stars kutua Tunisia, watatu kukosekana kikosini

Muktasari:

Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ iliyokuwa kambini nchini Uturuki itawasili Tunisia leo bila kuwa na wachezaji watatu tayari kuwakabili wenyeji keshokutwa katika mchezo wa kuwania kufuzu mashindano ya nchi za Afrika (Afcon) yatakayofanyika jijini Tunis.

Dar es Salaam. Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ iliyokuwa kambini nchini Uturuki itawasili Tunisia leo bila kuwa na wachezaji watatu tayari kuwakabili wenyeji keshokutwa katika mchezo wa kuwania kufuzu mashindano ya nchi za Afrika (Afcon) yatakayofanyika jijini Tunis.

Wachezaji hao ni Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na Adam Adam.

Stars chini ya Kocha Ettiene Ndayiragije itamkosa nahodha wa timu hiyo, Samatta anayeichezea Fernebahce kutokana na kuwa majeruhi huku wengine wakikosa visa za kuingilia Tunisia.

Naye Ulimwengu ambaye anaicheza TP Mazembe ya DRC atakosa mechi hiyo ya kwanza kwa timu hizo kutokana na kuchelewa kupata visa, hivyo atalazimika kuja jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuungana na wenzake kujiandaa na mechi ya marudiano. Kwa upande wa Adam wa JKT Tanzania alikosa visa baada ya kuchelewa kupata hati ya kusafiria wakati Shirikisho la Soka nchini (TFF) lilikuwa linashughulikia, huku muda wa kuondoka nchini ukimtupa mkono na timu kuondoka kwenda Uturuki.

Akizungumzia hali ya timu hiyo kutoka Uturuki jana, meneja Nadir Haroub ‘Canavaro’ alisema: “Maandalizi yanakwenda vizuri kuelekea mechi hiyo, hao (watatu) tutaonana nao Dar es Salaam. Timu itaingia Tunisia Jumatano (leo).”

Stars itawategemea John Bocco na Saimon Msuva katika ushambuliaji.

Kukosekana kwa wachezaji hao kumeelezwa kwamba ni pigo kubwa, ambapo mmoja wa wachezaji wa zamani wa Stars, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ alisema: “Mechi itakuwa ngumu na hilo linajulikana tunapokuwa tunacheza na timu zinazotokea ukanda wa huko, ugumu unaongezeka zaidi anapokosekana nahodha wetu Samatta.”

“Lakini kama Msuva na wachezaji wengine watakuwa katika hali nzuri, basi wanaweza kuziba pengo la Samatta ni muda wao wa kuonyesha kipaji, hiyo ya Ulimwengu na Adam kutokuwa na kikosi sina hakika nayo sana.”