Yondani arejeshwa Stars

Friday February 26 2021
yondanipic

Kelvin Yondani

By Thomas Ng'itu

KOCHA Mkuu wa timu ya Taif 'Taifa Stars' Kim Poulsen amewarejesha kikosini nyota Kelvin Yondani baada ya kukosekana kwa muda mrefu huku akimuita Yohana Mkomola kwa mara ya kwanza.

Poulsen leo Ijumaa Februari 26, 2021 ametangaza kikosi kinachojiandaa kucheza michezo ya kufuzu Afcon dhidi ya Equatorial Guinea na Libya mwezi ujao, Machi.

Yondani alikosekana katika kikosi kilichoshiriki CHAN mwaka huu nchini Cameroon huku akiwa miongoni mwa wachezaji waliofanikisha timu hiyo kufuzu mashindano hayo.

Inaelezwa sababu kubwa ya Yondani kuondolewa katika kikosi hicho ni baada ya kukosa timu alipomaliza mkataba wake na Yanga.

Kwa sasa nyota huyo anaichezea Polisi Tanzania ambayo alisaini mkataba wakati wa dirisha dogo la usajili msimu huu.

Upande wa Mkomola anayecheza soka la kulipwa nchini Ukraine katika klabu ya Inhulets Petrove inakuwa ni mara yake ya kwanza kucheza Stars tangu mara ya mwisho alipoichezea timu ya vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys).

Advertisement

Poulsen amesema katika kikosi chake amechanganya wachezaji wa timu za vijana lengo likiwa ni kuwapa muendelezo mzuri.

"Tunawatengeneza vijana kwa ajili ya kesho na ndio maana tunawapa nafasi pia wao ya kuwa sehemu ya kikosi kijacho cha timu ya Taifa".

Wengine walioitwa ni Aishi Manula, Metacha Mnata, Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Hassan Kessy, Israel Mwenda, Erasto Nyoni, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Carlos Protas, Kennedy Juma, Laurent Alfred, Mohamed  Hussein 'Tshabalala', Nickson Kibabage, David Bryson, Yassin Mustapha na Edward Manyama.

Viungo ni Simon Msuva, Hassan Dilunga, Ayoub Lyanga, Novatus Dismas, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude, Said Ndemla, Feisal Salum, Himid Mao, Ally Msengi, Baraka Majogoro, Salum Abubakary, Idd Seleman 'Nado', na Farid Mussa.

Washambuliaji Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta, Yohana Mkomola, Shaban Chilunda, Abdul Suleiman, Meshack Abraham, Ditram Nchimbi, John Bocco, Deus Kaseke, Kelvin John na Nassor Saadun.

Advertisement