Zoran: Dejan ni mtu na nusu

Zoran: Dejan ni mtu na nusu

KOCHA Mkuu wa Simba, Zoran Maki amesema akiwa kambini nchini Misri aliwaambia mabosi wake kuwa anahitaji straika mwingine mwenye kiwango bora zaidi ya waliokuwepo wakati huu ndipo wakamsajili Mserbia Dejan Georgijevic ambaye tayari ametangazwa juzi Jumapili.

 Straika huyo alikuwepo pia jana Jumatatu katika kilele cha Simba Day ambapo Simba ilicheza na St George ya Ligi Kuu ya Ethiopia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Zoran alisema akishirikiana na wasaidizi wake aliowakuta, walifanya uamuzi mgumu wa kuwatema Meddie Kagere na Chriss Mugalu kwa kuangalia viwango vyao vya msimu uliopita.

Alisema alipatiwa jina la Dejan akiwa Misri na baada ya kumuangalia kupitia video za mechi nyingi alizocheza pamoja na kuwauliza watu wake mbalimbali kutoka Serbia aliambiwa ni moja ya mastraika mzuri.

“Niliendelea kujiridhisha zaidi kupitia mechi mbalimbali ambazo Dejan amecheza naamini ni moja ya washambuliaji wazuri ambao watakuja kuongeza kitu katika safu ya ushambuliaji msimu ujao,” alisema Zoran na kuongeza;

“Dejan ana uwezo wa kufunga mabao aina mbalimbali akiwa ndani na nje ya boksi, msumbufu kwa mabeki, mikimbio yake ni kwenye maeneo sahihi, anaweza kutengeneza nafasi za kufunga pamoja na mambo mengi ya kimsingi nimeyaona kwake.

“Baada ya kuona ana sifa za kiufundi nilizokuwa nikizihitaji kwa mshambuliaji mpya nilimpitisha na kuwaeleza viongozi wamsajili kwani kiwango chake kitaongeza ubora wa kufunga.

“Nakumbuka wakati namuangalia Dejan nilipata majina ya washambuliaji wengine kutoka Ghana, Nigeria na Cameroon ila wote niliwakataa na kumtaka huyu kwani alinivutia zaidi,” alisema Zoran.