Zoran: Tulieni nyie, tumeshajua tatizo

SIMBA juzi ilianza vibaya msimu mpya wa 2022-2023 kwa kulala mabao 2-1 mbele ya watani wao, Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, lakini kocha wa timu hiyo, Zoran Maki amewatuliza mashabiki wao akisema wameshalijua tatizo.

Zoran aliyeiongoza Simba kwa mara ya kwanza kwenye mechi za mashindano na dabi yake ya kwanza tangu atue katika kikosi hicho, alisema Simba imepoteza mchezo huo kwa makosa ya mabeki wake wa kati kwa kufanya uzembe, sambamba na umakini mdogo wa safu ya ushambuliaji.

Katika mechi hiyo, Zoran aliwacheza Henock Inonga na Mohamed Ouattara aliyesajiliwa hivi karibu katika beki ya kati na kushuhudiwa straika wa Yanga, Fiston Mayele akitupia mara mbili na kuipa Yanga ushindi huo ambao ni wa pili mfululizo kwenye mechi za Ngao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Zoran alisema kipigo kimemfedhehesha na kuwaumiza wanasimba, lakini akawatuliza kwa kuwaambia wanajipanga na kurekebisha makosa kabla ya kuanza Ligi Kuu Bara na mechi nyingine zikiwamo za kimataifa ili kufanya vema.

Zoran alisema kutokana na ubora wa mabeki hao na uzoefu walionao si watu wa kufanya makosa mawili kama yale na kuwapa Yanga nafasi kwa urahisi kufunga mabao katika mazingira ambayo hayakuwa na shida.

Alisema katika mechi kubwa za dabi kama hizo unahitaji wachezaji walio na ubora ili kuwa na uamuzi wa haraka na Ouattara na Inonga ni miongoni mwao, ila kucheza kwa kujiamini kuliko kawaida ilikuwa ni kosa kubwa na madhara yake timu imepoteza.

“Kuna namna wenyewe wanatakiwa kuchukua hatua dhidi ya makosa hayo mawili hadi kusababisha kufungwa mabao na baada ya hapo kama kocha nitafanya kazi ya kuendelea kuwarekebisha ili kuwapa mbinu sahihi za kufanya wanapokuwa uwanjani,” alisema Zoran na kuongeza;

“Mechi tuliishika katika kipindi cha kwanza na tulikuwa na kila sababu ya kuimaliza ila wachezaji wangu kushindwa kufanya hivyo iliwapa nguvu Yanga kipindi cha pili na kujikuta tunapoteza mchezo.

“Hatukuhitaji kitu kikubwa zaidi ya kufunga mabao mengi katika kipindi cha kwanza ila tulishindwa kufanya hivyo wakati wenzetu Yanga walipata nafasi nne na mbili kati ya hizo wamefunga mabao, dabi ndio ilivyo inahitaji usahihi katika maeneo sahihi.

“Imetuumiza kama timu, wachezaji wangu wameniangusha baada ya kushindwa kupata ushindi katika mechi ambayo tulikuwa na uwezo wa kupata matokeo mazuri na kuchukua taji la kwanza msimu huu.”

Katika hatua nyingine, Zoran alisema kabla ya mchezo huo matarajio yalikuwa kuchukua taji la kwanza na kuwafunga Yanga ili kuvunja rekodi ya matokeo ya mechi kama hiyo msimu uliopita.

Zoran alisema walifanya maandalizi sahihi katika maeneo mengi ila bahati mbaya wachezaji wamemuangusha, lakini hilo limeisha, nguvu zote wakati huu zinaelekezwa katika mashindano mengine.

Alisema amekaa chini na wachezaji wake kuwaonyesha walipoteleza.