Ajibu, Sabilo wanukia Singida Big Stars

Muktasari:

  • SIKU chache tangu kupata ruksa ya kufanya usajili baada ya awali kufungiwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF), mabosi wa Singida Big Stars wameingia sokoni kwa kishindo na sasa wapo hatua ya mwisho kunasa saini za mashine mbili kutokea kwenye timu mbili tofauti, akiwamo Ibrahim Ajibu.

SIKU chache tangu kupata ruksa ya kufanya usajili baada ya awali kufungiwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF), mabosi wa Singida Big Stars wameingia sokoni kwa kishindo na sasa wapo hatua ya mwisho kunasa saini za mashine mbili kutokea kwenye timu mbili tofauti, akiwamo Ibrahim Ajibu.

Ajibu, aliyewahi kung’ara na Simba na Yanga kwa misimu tofauti, kwa sasa anakipiga Azam FC, ingawa hajaonyesha makali, lakini anatajwa kuwa hatua ya mwisho kutua timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu msimu huu kutoka Ligi ya Championship, sambamba na straika wa Mbeya City, Sixtus Sabilo.

Singida iliyokuwa kwenye kifungo cha kutosajili kwa msimu mmoja sambamba na Tanzania Prisons kwa kosa la kumsajili kipa Metacha Mnata wa Polisi Tanzania na Musa Mbisa wa Coastal Union wakiwa bado na mikataba na klabu zao, lakini hivi karibuni ilitangazwa kufutiwa adhabu hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya Singida inasema mabosi wa timu hiyo kwenye dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Desemba 15, litaanza na washambuliaji Ibrahim Ajibu wa Azam na Sixtus Sabilo wa Mbeya City.

Ajibu anamaliza mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Azam iliyomsajili dirisha dogo la usajili msimu uliopita akitokea Simba, huku ikionekana hakuna dalili ya kumuongezea mkataba mpya kutokana na kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Wakati huohuo, Kocha wa Polisi, Mwinyi Zahera ameonyesha nia ya kumtaka Ajibu, akiamini ni kati ya wachezaji wenye vipaji na aliwahi kufanya naye kazi Yanga akionyesha ubora hadi Simba ikamsajili.

Sabilo aliyesajiliwa na Mbeya City msimu huu akitokea Namungo amebakiza mkataba wa miezi sita kuitumikia timu hiyo kama Singida itamsajili italazimika kulipa kiasi hicho cha pesa kuvunja mkataba wake.

Hadi duru la kwanza linamalizika, Sabilo amefunga mabao saba na kuasisti sita akiwa amehusika kwenye mabao 13 kati ya 20 yaliyofungwa na timu nzima msimu huu.

Singida ikifanya maboresho hayo kwenye kikosi chake inaelezwa huenda ikaachana na nyota wake wawili wa kigeni washambuliaji, Peterson Cruz na Miguel Escobar.

Kocha wa Singida, Hans Pluijm alisema dirisha dogo la usajili watafanya maboresho machache, ni muhimu kuwa na maingizo mapya.