Azam nayo inautaka ubingwa

AZAM FC inaonekana kuupania ubingwa wa Ligi Kuu Bara kutokana na matokeo mazuri wanayoendelea kuyapata hadi sasa huku kiungo wa timu hiyo, Isah Ndala akisema ubingwa ndiyo lengo lao msimu huu.

Azam msimu huu imeonyesha ushindani mkubwa kwenye Ligi sambamba na kufanya usajili mkubwa kwa kusajili wachezaji wenye viwango vizuri kama Ndala, James Akaminko, Tape Dinho, Kipre Junior ili kuongeza ushindani kwenye kikosi chao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ndala alisema; “Sitaki kuzungumzia kuhusu mwenendo wa timu zingine, acha tuendelee kupambana hadi mwisho wa msimu kisha ndio tutaangalia nani yupo na wengine wapo wapi.”

Ndala alisema siri kubwa ya wao wachezaji kupambana ni kutokana na uwepo wa Kocha Kally Ongala anayewafanya waishi kama familia na hilo limechangia kwa kiasi kikubwa wawe na kiwango kizuri.

“Hapa ni kama familia kwa hiyo kuna muda hata kwenye kucheza tuna furaha kwa yule ambaye ataanza kwa sababu kocha ana imani kubwa sana na wachezaji wote,” alisema.

Akizungumzia upande wake kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza alisema; “Nasali, mazoezi na kutaka kufanya kitu ambacho kitakuwa na utofauti kila siku.”

Azam inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 32 ikicheza mechi 14 na ikishinda 10, kupoteza mechi mbili na kutoka sare mbili huku ikifunga mabao 21 na kufungwa 13.