Aziz KI alivyoshuhudia tetemeko Morocco

Dar es Salaam. Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Azizi Ki amewatoa hofu mashabiki kuhusiana na hali yake baada ya tetemeko la aridhi lililotokea nchini Morocco, huku akitumia nafasi hiyo kutoa salamu za pole kwa waathirika.

Aziz Ki alikuwa nchini Morocco na timu yake ya taifa, Burkina Faso kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa kufuzu kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Uswatini, uliochezwa kwenye Uwanja wa Marrakech, mjini Marrakesh (Morocco) uliomalizika kwa suluhu.

Akizungumza sakata zima la tetemeko hilo, Aziz Ki alisema haikuwa hali ya kawaida, kwani timu nzima ya taifa ilikuwa hotelini baada ya mchezo, ndipo walipoanza kusikia hali ya tofauti, wakati tetemeko hilo lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 2000.

Nyota huyo mwenye mabao manne msimu huu alisema walihisi kishindo na kuanza kuulizana kilichotokea, kabla ya kuchungulia nje na kushuhudia majengo yakiporomoka na wao kuanza kujihami.

"Haikuwa hali ya kawaida, ulikuwa ni mshituko mkubwa benchi la ufundi lilifanya kazi kubwa kuhakikisha wanatukusanya pamoja ili kukwepa adha ya kuanza kutafutana mmojammoja na baada ya tukio hilo walitujenga kisaikolojia ili kutuondoa kwenye hali ya taharuki.

"Haikuwa rahisi, kwani kila mmoja alikuwa anatafuta njia yake ya kujiweka kwenye usalama, lakini viongozi wa timu yetu hawakuwa nyuma kutuweka pamoja ili tuweze kupata nafasi ya kuzungumza na kusahau kilichotokea," anasema Aziz Ki.

Nyota huyo mwenye miaka 27, alisema amepokea simu nyingi kutoka kwa viongozi, marafiki familia na ndugu wa karibu ambao walitaka kupata ufafanuzi kuhusiana na tukio lililotokea huko.

"Haikuwa rahisi kupokea simu kwa muda huo, kwani mambo yalikuwa ni mengi, lakini mara baada ya muda tuliruhusiwa kushika simu ili kuzungumza na familia kuwatoa kwenye hali ya taharuki.

"Natoa pole kwa familia zilizoathirika na tukio hilo na kuwaombea majeruhi Mungu awape nafuu warudi kwenye hali zao za kawaida, pia nawashukuru watu wote walionitafuta na kunijulia hali, nipo salama mimi pamoja na wachezaji wenzangu," alisema mshambuliaji huyo.

Akizungumzia suala la kurudi Tanzania, Ki alisema anausikilizia uongozi wa Yanga ambao uliahidi kusimamia kuona anarudi kwa uharaka ili kuuwahi mchezo wa Jumamosi dhidi ya Al Merreikh.

"Ndege ambayo nilikata kwa ajili ya kurudi Tanzania imeahirisha safari kutokana na tatizo hili, hivyo nasubiri kama kuna utaratibu mwingine unaofanyika," aliongeza.

Ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema tayari Aziz Ki amefanikiwa kutoka sasa yupo Ufaransa na leo saa 3 usiku atacheza mechi ya kirafiki na Morocco na baada ya hapo ataungana na timu moja kwa moja Kigari, Rwanda.

"Ki ameshaondoka Morocco, yupo salama na leo usiku atakuwa na mchezo wa kirafiki wa Burkina Faso na Morocco na baada ya hapo atapanda ndege ambayo inamuelekeza kuja moja kwa moja Rwanda," alisema Kamwe.

Rais Samia Suluhu Hassan alitoa salamu za pole kwa watu wa Morocco huku akiungana nao katika kipindi hiki kigumu.

“Habari za kushtusha kutoka Morocco kutokana na tetemeko la ardhi. Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Tanzania, natoa salamu za rambirambi kwa Mfalme Mohammed VI, familia za wafiwa na wananchi wote wa Morocco katika kipindi hiki kigumu. Maombi yetu yako pamoja nanyi,” alisema.