Baba: Sure Boy piga mzigo!

Monday December 27 2021
surepic
By Olipa Assa

BABA mzazi wa kiungo mpya wa Yanga, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Abubakar Salum amekiri mwanae anaenda kukutana na changamoto mpya, ila akampa maujanja wa kutoboa mbele ya mastaa anaokutanao Jangwani.

Sure Boy mkubwa aliyasema hayo jana alipotafutwa kueleza hatua ya mwanae kujiunga na klabu aliyoichezea kwa mafanikio makubwa naye alisema licha ya ushindani wa namba kikosini, Sure Boy mdogo anatakiwa kupiga mzigo kuliko alivyokuwa Azam ili kujijengea heshima.

Winga huyo wa zamani aliyewahi pia kutamba na timu za Sigara, Tanzania Stars na Taifa Stars, alisema anatambua ndani ya Yanga eneo la kiungo analoenda kucheza kijana wake lina ushindani mkali, lakini anamwamini ni mpambanaji anayeenda kuonyesha kipaji.

“Najua anatambua soka linahitaji nini, amejiunga na timu iliyo na mashabiki wengi, muhimu kwake ni kujituma kwa bidii kwa nidhamu kubwa ndani na nje ili kusuuza roho za wanayanga waliomuamini na kumsajili,” alisema Sure Boy na kuongeza; “Nimefurahi amejiunga na Yanga, ila hii haihusiani na yale maneno eti ni shabiki wa kutupwa, kiasi cha kucheza kinazi akikutana nao. Dogo ameifunga Yanga mara mbili na Simba hajaifunga.”

Aliushukuru uongozi wa Azam kumalizana na mwanae kiroho safi kwa kuthamini mchango wake ndani ya timu hiyo aliotwaa nao mataji karibu 10 akiwa mchezaji mwandamizi.

Advertisement