Baba wa Ansu Fati afunguka mazito

Barcelona, Hispania. Matumaini ya Manchester United kuipata huduma ya nyota wa Barcelona, Ansu Fati yamezidi kuwa makubwa baada ya hivi karibuni baba mzazi wa nyota huyo, Bori Fati kumwambia kwamba aachane na timu hiyo.

Ansu Fati, ambaye alionekana kuwa mmoja kati ya nyota wanaoweza kuziba pengo la Lionel Messi, msimu huu amecheza mechi 24 za La Liga, ambazo nyingi kati ya hizo aliingia akitokea benchi.

Hata hivyo, Fati mwenyewe anatamani kuendelea kusalia kwenye kikosi hicho na kupambania nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Wakati huo huo, wakala wake pia, Jorge Mendes ameshaanza mazungumzo baadhi ya wawakilishi wa timu mbalimbali barani Ulaya ili nyota huyo ajiunge nazo baada ya msimu huu kumalizika.

Baba mzazi wa staa huyu alikuwa kwenye mkutano na mabosi wa Barca mwanzoni mwa wiki hii na baada ya kikao hicho amesema kwamba hakuna namna Ansu Fati inabidi aondoke Barca ili kulinda kipaji chake kwa kuwa hata yeye haelewi kwanini hapewi nafasi ya kucheza.

Akizungumza na tovuti ya El Partidazo baba mazazi wa nyota huyu alisema: “Inanikera jinsi ambavyo wanamchukulia Ansu, wanampa dakika moja, mbili au tatu, nachukizwa na hali hii na naamini anahitaji muda mwingi zaidi wa kucheza.

“Kwanini Xavi hampi nafasi yakucheza zaidi? Mimi sina jibu, lakini kama baba inaniuma na nimeshamwambia Ansu kwamba anatakia abadilishe timu ikiwa anataka kufanikiwa lakini hataki kunielewa, anahitaji kuendelea kucheza Barcelona.”

Ansu Fati ni miongoni mwa wachezaji waliokuzwa kwenye akademi ya Barcelona akitokea Sevilla na alipandishwa kwenye kikosi cha kwanza Septemba 23, 2020.

Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2027.