BAHANUZI: Maisha yangu Mungu anajua

Monday January 25 2021
Bahanuzipic
By Olipa Assa

JINA la straika wa zamani wa Yanga, Said Bahanuzi (30) lilikuwa linatamba kwa wadau wa soka nchini, baada ya kusajili ndani ya kikosi hicho msimu wa 2012/14, je unajua siri yake? Msikie mwenyewe anachosema.

Bahanuzi mwenye asili ya Rwanda anasema jina Bahanuzi kinyarwanda lina maana ya mtu mkubwa katika jamii, anasisitiza hakushangazwa na kuvuma ghafla alipotua Yanga.

“Mimi ni mchanganyiko, mama ni Msukuma na baba ni Mnyarwanda, licha ya Yanga kunitambulisha kwa jamii, ila hata mtaani nilikuwa nikicheza basi nakuwa maarufu vile vile,” anasema.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Bahanuzi anafunguka vitu vingi ikiwemo sababu ya kukaa nje ya soka, ndoa ilivyomtenganisha na watoto wake na anajikuta anaishi kama mkiwa kwa kila kitu kwenda ndivyo sivyo.

“Maisha ni safari ndefu, nimepitia mengi yanayoumiza moyo wangu na watu wanaonizungumzia kila wanachoweza hawanijui, wakati mwingine naona taarifa zangu kwenye mitandao ya kijamii nabakia nashangaa tu na kushukuru Mungu, nikiamini ipo siku ukweli wote wataujua,” anasema.

Kupitia gazeti lako pendwa la Mwanaspoti, utayajua mengi ambayo mchezaji huyo anayazungumza kuhusu soka na maisha yake binafsi, yalivyofanyika mwiba kwenye maisha yake.

Advertisement


MAISHA NDANI YA YANGA

Yanga ilimsajili Bahanunzi msimu wa 2012/14 akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro, anaeleza awali alikuwa muoga kutokana na ukubwa wa klabu hasa kwa upande wa mashabiki namna walivyokuwa wanamchukulia kwa ukubwa, uliomfanya awaze mara mbilimbili jinsi ya kufanya kinachotarajiwa kwake.

Anasema baada ya muda mfupi alizoeana na wachezaji aliowakuta klabuni hapo na kwamba ilimuongezea kujiamini na akawa anafunga kwa fujo mechi za kirafiki ambazo Yanga ilikuwa inacheza kujiandaa na msimu mpya.

“Nilianza kuonekana rasmi kwenye mechi za mashindano hasa Kombe la Kagame na mechi yangu ya kwanza ilikuwa ni dhidi ya Vital’O ya Burundi, niliingia dakika ya 78, tulishinda mabao 2-0, mechi zilizofuata zote nilianza na kucheza dakika 90 na nilikuwa nafunga ,” anasema Bahanunzi na anaongeza kuwa,

“Mashindano ya Kagame ndio yalioling’arisha jina langu, nakumbuka niliibuka mfungaji bora, baadae ikafuata mechi ya ngao ya jamii, kisha tukaingia kucheza Ligi Kuu Bara, ikawa mwanzo mwingine wa maisha yangu kubadilika taratibu, kutoka kwenye furaha na kuingia kwenye huzuni iliyokuwa imebakia moyoni,”anasema.

Anaendelea kusimulia kuwa majukumu ya Ligi Kuu Bara, yalianza ambapo alicheza mechi tatu bila kufunga bao, hapo kasheshe ilimpata hadi kufikia hatua ya kuitwa na viongozi wake, makao makuu ya klabu yaliopo Jangwani, Dar es Salaam.

“Maneno yalikuwa mengi yaliyonizidi uwezo na umri wangu, nakumbuka niliitwa na viongozi wa Yanga wakaniuliza kwanini hufungi? Niliwajibu ligi ndio imeanza 2013/14, ajabu wakaniambia umeanza starehe za wanawake ndizo zinakutoa kwenye reli, ilinishitua na kuniumiza, ilinibidi ninyamaze kwa kuwaheshimu,” anasema na kuongeza kuwa,

“Kilichoendelea nikawa sipangwi kwenye mechi, huku tetesi za kuniita malaya zikiwa zinazidi kuendelea zaidi hadi kufikia hatua ya mke wangu kujisikia vibaya na kuwa mwenye wivu ambao ulinikosesha madili mengi ya matangazo, akidhani ndio ningepotea zaidi,” anasema.

PENALTI ILIMUONDOA

KWENYE RELI

Anakiri kwamba mwaka 2014, kitendo chake cha kukosa penalti ya ushindi dhidi ya Al Ahly ya Misri, mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kilichangia kumuondoa kwenye ndoto za kufika mbali.

“Penalti ilizua nongwa, wakati bado nipo Misri nilipigiwa simu mashabiki wamekwenda kufanya fujo nyumbani kwangu, huku wakitukana matusi ya kila aina, mke na watoto walikuwa ndani na kama haitoshi wakati tunarudi hakuna mchezaji aliyekuwa ananiongelesha, kali zaidi ni matusi niliyopokewa nayo Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julias Nyerere, nikanyamaza kimya nakuomba Mungu tu,” anasema na anaongeza kuwa,

“Nilijihisi mkosaji nisiyestahili kusamehewa, roho ya kuacha soka ilinivaa, aliyenisaidia ni kiongozi, Hussein Ndama alinikalisha chini, akanijenga na kuniambia haikuwa ridhiki yako, himili mtikisiko unaokupata, nakumbuka siku hiyo alinipa dolla 500, kwani aliona jinsi wenzangu walivyokuwa wanapewa pesa na mashabiki halafu mimi nilinyimwa,” anasema.

Anaendelea kusimulia kuwa siku ya pili wakati wachezaji wenzake wanaogopa kwenda mazoezini ambayo yalifanyika Uwanja wa Kaunda, uliopo makao makuu ya klabu hiyo, aliamua kuwahi mapema 9:00 jioni na muda sahihi wa kuanza ilikuwa ni saa 10:00.

“Siku hiyo mashabiki walijaa mapema sana, baada ya kufika wachezaji wenzangu, kuna shabiki aliniita nitoke uwanjani, nikatoka kisha akanipeleka katikati ya mashabiki, akawauliza huyo anaitwa nani, wakaitikia ‘Bahanuzi’, hapo mwili wangu ulikuwa unavuja jasho huku nasikia ubaridi wa ajabu,” anaongeza,

“Akawauliza tena tumsamehe ama tusimsamehe, wakajibu tumemsamehe, baadae wakanipa maneno, wakuniambia nipunguze wanawake, ilinibidi kuwa mpole kwasababu nilikosa penalti, kisha wakaniambia haya nenda kaendelee na mazoezi, nikaenda kujiunga na wenzangu, huku moyo wangu ukijaa unyonge kuona nabaguliwa,” anasema.

Anasema penalti hiyo ni kama ilimtia nuksi, kwani hakubahatika kupangwa mpaka alipokuja kocha Mbrazil Marcio Maximo, aliyemkalisha kitako na kumwambia jinsi anavyotuhumiwa kuhusu penalti na wanawake.

“Jambo kubwa aliniambia nimeambiwa wewe unahangaika sana na wanawake, umesahau kazi yako, lakini ulikosa penalti, nakutia moyo hata mimi niliwahi kukosa uwanja mkubwa wa Brazil mara tano, soka lipo tofauti na siasa zao, piga mazoezi nione kipaji chako wanachokisema kinafifishwa na wanawake,” anasema na anaongeza,

“Alipenda nilivyokuwa nayafanya mazoezi akanipa nicheze mechi iliyofuata kila mtu akabaki anashangaa na akasema inabidi nipuuzie kinachosemwa na mashabiki na viongozi kuhusu tuhuma nilizokuwa napewa, mpaka wakamwambia nina mwanamke mnene aliyenizidi kila kitu,”anasema.

Anasema bado mambo yaliendelea kuwa magumu kwani Maximo baadae alimwambia atakuwa straika namba tatu wa kwanza akiwa ni Jerry Tegete na wa pili, Gerson Jaja ambaye alitoka naye Brazil kwa lugha nyingine ni kwamba angekuwa anakaa jukwaani kushuhudia wenzake wakifanya kazi.

“Nilivyoona hivyo nikamuomba kocha niende kwa mkopo kwani tayari, Polisi Moro walikuwa wanahitaji huduma yangu, niliiona hiyo ni fursa ya kujipanga kwa kucheza muda mrefu, ambako nilijengeka kuwa fiti na akili ilikuwa inawaza kazi badala ya maneno,”anasema na anaendelea kusimulia,

“Muda ambao nilicheza Polisi Moro, nilichukua zawadi ya mchezaji bora mara mbili ya mwezi, kuhusu zawadi za hapa na pale zilikuwa nyingi, ikiwemo simu janja niliyopewa na mtu kama moja ya kufurahia kazi yangu,”anasema.

Ukiachana na furaha yake ya kucheza Moro, anasema alimkuta kocha Mohammed Rishard ‘Adolf’ akiwa kocha wa timu hiyo, anaeleza ndiye aliyemjenga na kumwambia afanye kazi bila kuangalia ukubwa wa timu, aliyotoka bali afahamike kwa kiwango kizuri.

“Ni kocha ambaye anajua kufundisha mbinu, angalia timu anazofundisha akifungwa ni bao moja tena kwa shida, hicho kitu nilikiona wakati nipo Polisi Moro,” anasema na anaongeza kuwa,

“Ni kweli Yanga walinipangia nyumba ya kifahari ila nilikuwa nakosa usingizi, tofauti na maisha ambayo niliishi Polisi Moro, ambako licha ya kuishi sehemu ya kawaida, lakini nilikuwa na furaha ambayo akili yangu ilikuwa inawaza kazi na sio maneno,”anasema.

Mbali na penalti kumuondoa kwenye reli, anakiri kwamba utoto pia ulichangia kwasababu kila kitu alikuwa anakiweka wazi, huku wenzake wakivitumia kama fimbo ya kumuumiza kuhakikisha hafanikiwi kwa njia yoyote ile.

“Nakumbuka kuna mchezaji aliniambia Said, ukitaka kuendelea kucheza Yanga nenda kwa mganga wa kienyeji, lasivyo huo utakuwa mwisho wako wa kucheza soka, lakini nilikuwa najiuliza ninakwenda kufanyaje, nilikuwa sipati jibu.”

Je, Bahanuzi alifuata ushauri aliopewa na mwenzake wa kwenda kwa mganga wa kienyeji? Maisha yake ya sasa yapo vipi na anafanya nini? Usikose majibu ya haya yote kesho Jumatatu.
anasema ana anaongeza kuwa,

“Kuna siku wakati nipo kambini Yanga, nilikumbwa na tukio la ajabu, wakati nipo chumbani majira ya jioni hivi ulikuja upepo mkali, ukaangusha dirisha, katika mazingira ambayo sikuelewaelewa,” anasema na anaendelea kusimuliwa kuwa.

“Nilikimbia kwenda kumwambia nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliniambia niende nikakae naye kwenye chumba chake, nikashuka chini ambako alikuwa anakaa yeye, baadae soksi ambazo zilipotea nikazikuta mlangoni kwangu wakati natoka, kifupi nilikumbana na mengi ambayo siwezi kumaliza kuyasimulia, ndio maana nasema wanaonisema vibaya hawajui ukweli na wanaojua ukweli wamenyamaza kimya,”anasema.

Anasema kutokana na kukumbana na matukio mbalimbali ya kumtisha, yalimfanya mwili aishi Yanga, lakini akili yake iwe sehemu nyingine ambayo alikuwa anaitamani akakae kwa amani.

“Yanga niliifurahia mwanzoni, baadae nilikuwa naumia moyoni, mashabiki hawakujua undani wa maisha yangu zaidi ya kunituhumu na umalaya, ambao niliishia tu kushangaa, kiukweli hilo lilikuwa linanitesa sana,”anasema.


YANGA YAMBANIA SIMBA

Anasema wakati yupo Polisi Moro, uongozi wa Simba ulimfuata kuhitaji huduma yake, lakini tayari alikuwa ameiongeza mkataba wa miaka miwili, hivyo akawa amebakiza mwaka mmoja na miezi sita, uliokuwa unamzuia kufanya mazungumzo na timu nyingine.

Anasema baada ya kuipokea ofa ya Simba, aliupigia uongozi wa Yanga kuuambia ana ofa aliyonayo bila kutaja ni timu gani, lakini alijibiwa bado yupo kwenye mipango yao.

“Waliniambia wana uhitaji na mimi, ajabu nikakataa ofa ya Simba, nikiwa likizo nikaona jina langu ni kati ya wachezaji wanaoachwa, wakavunja mkataba ambao hawajanilipa hadi leo wa mwaka mmoja na miezi sita,”anasema na anaongeza kuwa,

“Japokuwa Simba ilinipuuza kunisajili kabla ya kusaini Yanga kwa mara ya kwanza, alikuja kiongozi alikuwa anazungumza na mimi kwa dharau sana, ila nikashukuru Mungu kwa kila jambo,”anasema.


AFICHUA LA MOYONI

Bahanunzi ambayee ni wa pili kuzaliwa kati ya watoto sita, anafichua siri ya moyoni mwake kwamba ndoto yake kubwa, ilikuwa kucheza Simba ambayo inashabikiwa na wazawa wake, hivyo aliamini kupitia kipaji chake, angeweza kuwapa furaha wakati akifunga.

“Sina maana kwamba Yanga sikucheza kwa moyo, lakini nilikuwa nikirudi nyumbani nikimwambia mama hamia Yanga, alikuwa anasema nakujali sana kijana wangu na kukutakia mema ya kazi yako, ila siwezi kushabikia Yanga, hivyo mpaka leo mama yangu anakwenda uwanjani kuangalia mechi za Simba inapocheza,” anasema na anaongeza kuwa,

“Sababu nyingine Simba ilikuwa inamfanya atamani kuichezea ni kutimiza ndoto ya kwenda kucheza nje ya nchi, jambo hilo Yanga halikuwepo kwa miaka ya nyuma, kuwaruhusu wachezaji wake kutoka ,”anasema.


MILIONI 600 ZAIKIMBIZA TP MAZEMBE

Anasimulia jinsi ambavyo dili la kutakiwa na TP Mazembe lilivyoyeyuka, kutokana na Yanga kuhitaji pesa ndefu, zilizokuwa haziendani na uhalisia wa uzoefu na jina lake.

“Wakati nipo Yanga, uongozi wa TP Mazembe ulinifuata, lakini walihitaji Sh 600 milioni, kiukweli ilinishitua sana kwani wao walinisajili kwa Sh 12 milioni, nikitokea Mtibwa Sugar, ni kweli nilikuwa na kipaji lakini sikucheza kwa muda mrefu wa kuhitaji kiasi kile,” anasema na anaongeza kuwa,

“Yanga kipindi hicho walikuwa wagumu kuwaachia mastaa wao kwenda kujaribu maisha nje, badala yake walikuwa wanainua vikwazo, kama vilivyonipata, zilikuja timu nyingi kutoka Misri na China, lakini ziligonga mwamba,”anasema.


WATOTO WAKE KUCHEZA MTIBWA SUGAR

Anasema baada ya kuachana na Yanga, alirejea Mtibwa Sugar, anayoitazama kama inajua kulea wachezaji licha ya kupata kipato kidogo, hilo ndilo linamtamanisha siku moja watoto wake wakikua waje kuichezea timu hiyo.

Bahanuzi ambaye ni baba wa watoto watatu aliowataja kuwa ni Samir (7), Sabra(5) na Azir (1 na miezi 6) anasema “Kijana wangu wa kwanza anapenda sana mpira, ninatamani siku akikua aje aanzie Mtibwa Sugar, ndipo aende timu nyingine,” anaeleza.


KINACHOMUUMIZA

Anasema baada ya kuondoka Yanga, timu ya mwisho kuichezea ni Mtibwa Sugar msimu wa 2016/17 ambako aliumia goti la mguu wa kulia ambapo mfupa umekaa pembeni, hivyo anajikuta goti linajaa maji.

Anasimulia kwa uchungu wa kutoa machozi kwamba, gharama za matibabu kwenda kufanya matibabu nchini Afrika Kusini zimemshinda, hivyo wakati mwingine akifanya kazi kwa muda mrefu goti linajaa maji na kumsababishia maumivu makali.

“Naumia kwasababu sijatimiza ndoto zangu kwenye soka, naishia kuwatazama wachezaji wenzangu wakifanya kazi, nimehangaika sana hospitali jibu ninaloambiwa ni moja, unapaswa kwenda kufanyiwa upasuaji Afrika Kusini, najiuliza haya maji yanayojaa mguuni, itakuaje kufanya shuguli za kuendesha maisha yangu, sipati mwanga wa jibu,”anasema

Anasisitiza kwamba alichokizungumza ndio sababu ya yeye kuwa nje ya kazi ya soka na kwamba laiti kama angetibiwa angeendelea kucheza ama kwenda kusomea uchambuzi wa soka, huku akifurahishwa na umahili wa uchambuzi wa Ally Mayay na Mwalimu Alex Kashasha.

“Kama atatokea mtu mwema atanisaidia kuondoa tatizo langu ambalo nikilala na kuamka huwa nawaza sana, nashindwa kujua mwisho wangu, nitashukuru kwani natamani afya yangu kuiona inakuwa sawa,”anasema.


STARS 3, WATANI MOJA

Anasema kwa muda ambao alicheza Yanga aliitwa kwenye Stars mara tatu na kucheza mechi ya watani wa jadi mara moja, huku nyingine akiwa anasugua benchi.

“Nakumbuka mechi ya watani wa jadi ambayo nilipewa nafasi ya kucheza msimu wa 2013/14 ilikuwa tafu sana, upande wa Simba golini alikaa Juma Kaseja, mabeki walikuwa Juma Nyoso, Shomary Kapombe na Masoud Nassor ‘Chollo’ hao watu walijua kukaba, lakini tulipambana iliisha sare ya bao 1-1,”anasema.

Anasema ndoto zake ilikuwa ni kuitumikia kwa muda mrefu timu ya Stars, lakini anaona haikuwa ridhiki aliyopangiwa na Mungu wake, kilichobakia ataendelea kuwatazama wengine na kuwaombea.


FAMILIA IMETAWANYIKA

Anasema pamoja na kupata majaribu ya kila aina kwenye kazi yake ya soka, katika ndoa yake kuna moto hadi ameamua kuondoka nyumbani kwake kuepusha kudhuliana na mke wake.

“Nimepitia vitu vingi vigumu, nilitamani nipate faraja ya watoto na mke, nako mambo yamekuwa tofauti, niliondoka nyumbani takribani mwaka sasa, sijawaona watoto na imekuwa ngumu kuongea nao, inaniumiza sana kiasi kwamba namuomba Mungu anisimamie, maana nikipiga simu ninachoambulia nakistili,” anasema na anaongeza kuwa,

“Wanaonisema na vitu ambavyo sipo navyo hawanijui, siwezi kuzungumzia kiundani maana ni suala la kifamilia, ila ndio hivyo naumia kukaa na watoto wangu utadhani baba yao nimefariki wakati nipo hai, lakini ndio maisha na najifunza namna binadamu tulivyo,”anasema.


SOKA LIMEMPA NINI

Anasema soka limempa mashamba anayolima, mchele, iliki na mihogo, lakini pia ana nyumba na viwanja.

“Kwasasa nipo najilimia mashamba yangu kwa ajili ya chakula na kupata pesa za kujikimu kimaisha na kilimo nakifanyia nje ya Dar es Salaam,”anasema.


KIKOSI CHAKE BORA

Anataja kikosi chake bora kwenye Ligi Kuu Bara kwasasa kuwa kipa ni Aishi Manula (Simba), Shomary Kapombe (Simba), Issa Rashid ‘Baba Ubaya (Mtibwa Sugar), Bakari Mwamnyeto (Yanga), Agrey Moris (Azam), Jonas Mkude (Simba), Abrahim Mussa (Ruvu), Feisal Salum ‘Fei Toto (Yanga), John Bocco (Simba) na Miraji Athuman (Simba).

“Kwa kocha mzawa anayefanya vyema kwasasa na ana kikosi kizuri ni wa Ruvu Shooting, Boniface Charles Mkwasa, nimeona jinsi ambavyo wachezaji wametulia na wanapambana,” anasema.


Advertisement