Barbara: hii ni trela, mengi yanakuja

Tuesday November 30 2021
trelapic
By Ramadhan Elias

BAADA ya kuanza kurejea katika makali yake siku za hivi karibuni, uongozi wa Simba umesema hii ni trela tu kwa sbabu mengi mazuri yanakuja kwamba wamejipanga kuendeleza walipoishia msimu uliopita.

Jana imeipasua Red Arrows ya Zambia 3-0 kwenye mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika na sasa hesabu imezihamishia kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara Desemba 1, dhidi ya Geita Gold kabla haijapaa kwenda Zambia kumaliza kazi kwa Arrows na kutinga makundi.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez, Simba ya msimu huu imejipanga kote kote yaani ndani na nje ya uwanja kuhakikisha inapata ushindi kwenye kila mechi ili kutimiza malengo iliyojiwekea ambayo ni kutwaa ubingwa wa ligi na kufika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuteleza kwenye Ligi ya Mabingwa.

Barbara ambaye anaiendesha timu hiyo kidijitali alisema; “Kama viongozi wa Simba sisi tunataka ushindi, tupo imara zaidi msimu huu na tunataka kuwakilisha nchi yetu kimataifa kama tulivyofanya misimu iliyopita na hilo tunalifanyia kazi kwa ukubwa zaidi.”

Alisema kwa sasa Simba ndiyo timu kubwa Afrika Mashariki na Kati ndio maana na kila timu inayocheza dhidi yao inakomaa sana ili kujiongezea thamani na wachezaji wake kuitumia kujitafutia soko, lakini wao wako tayari kwa hilo na wanazichukulia mechi zote kwa uzito sawa.

“Hatudharau timu yeyote, kila mechi tunayoicheza kwetu ni fainali kwani timu pinzani zinazocheza na sisi zinapambana kwa ubora zaidi ili kujitafutia soko sababu wanajua Simba ndio kwenye maisha bora zaidi, hivyo tumejipanga kupambana nao ili tuzidi kuwa bora na kupata mafanikio zaidi kifedha, makombe na kupeperusha bendera ya nchi kwa ujumla,” alisema Barbara.

Advertisement
Advertisement