Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Beki Yanga aula Asa Tel Aviv

Muktasari:

  • Mchezaji wa Twiga Stars na Yanga Princess, Noela Luhala amejiunga na Asa Tel Aviv ya Ligi Kuu ya Wanawake Israel kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Dar es Salaam. Nyota wa Twiga Stars ambaye msimu uliopita aliitumikia Yanga Princess, Noela Luhala ameandika historia mpya baada ya kujiunga na Asa Tel Aviv inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Israel kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Usajili huo unamfanya Noela kuwa mchezaji wa kwanza wa kike wa Tanzania kusajiliwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu Israel, Mwananchi imethibitisha.

Kabla ya kukamilisha usajili huo, Noela alikuwa akiwindwa na timu mbalimbali hapa chini zikiwemo Fountain Gate Princess na Simba Queens.

Beki huyu wa kati ambaye anaweza pia kucheza nafasi ya beki wa kulia alikuwa nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ya wanawake chini ya miaka 17, kilichofuzu na kushiriki Kombe la Dunia India mwaka 2022 na kufika robo fainali.

Mwananchi linafahamu kwamba, Noela alikuwa akiwindwa na timu mbili za Israel, ambapo mbali ya hiyo aliyojiunga nayo alikuwa akihitajika  na  Hapoel Tel Aviv.

Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa Noela mweye umri wa miaka 18, kutoka nje ya mipaka ya Tanzania kucheza soka la kulipwa Ulaya akiwa anaungana na mastaa wa kike wengine wa Tanzania wanaocheza Ulaya ambao ni Aisha Masaka, Oppa Clement na Diana Msewa.

Baada ya kukamilisha dili hilo Noela anatarajiwa kufunga safari ya kwenda Israel ndani ya wiki mbili kuanzia sasa.

Noela ambaye alianza kucheza soka katika timu ya Mapinduzi Queens, alijiunga na Yanga mwaka 2021 ambapo amedumu kwa misimu mitatu kabla ya kuachana nao mwisho wa msimu uliopita.

Asa Tel Aviv ni timu inayomilikiwa na Chuo Kikuu cha Asa kilichopo Tel Aviv ambayo ni miongoni mwa timu zenye mafanikio makubwa katika soka la wanawake nchini Israel.

Timu hiyo imeshinda mataji nane ya Ligi Kuu ya Israel na imechukua makombe saba ya Chama cha soka cha Israel na inatajwa kuwa timu ya wanawake yenye idadi kubwa ya mashabiki nchini humo.

Ni timu ambayo imeshiriki mara nane tofauti katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa wanawake ingawa haikufanikiwa kufika hatua za juu.