Bocco: Tumejipanga vizuri kushinda kesho

Friday March 05 2021
BOCCO PIC
By Thobias Sebastian

Khartoum. Nahodha wa Simba, John Bocco amesema morali na hali ya ushindani katika kambi yao ipo juu wanasubiri tu muda wa mechi uweze kufika ili kuipigania timu.

Bocco alisema wamefanya mazoezi yao ya mwisho jioni hii na maandalizi ya uwanjani yote kiujumla yamekwenda vizuri tayari kwa kuibuka na ushindi.

"Tunamuomba Mungu kesho atuamshe salama ili wale ambao watapata nafasi ya kiuwakilisha timu katika dakika 90, wafanye kazi iliyotuleta hapa.

"Hali na morali ya wachezaji ambao tupo hapa zipo juu kwa ajili ya kuona tunashinda mechi nyingine ya ugenini kama ambavyo ilivyokuwa ile ya DR Congo.

"Kuhusu rekodi na matokeo ya mechi zilizopita haziwezi kuchukua nafasi wakati huu kwani tunatambua tunakwenda kucheza mechi ngumu ambayo tunahitaji kushinda," alisema Bocco.

Katika hatua nyingine Bocco alisema kushinda kwao mechi mbili haina maana kwamba wanaweza kuvuka mafanikio yao ya msimu wa 2018-19 walipocheza mashindano hayo.

Advertisement

Bocco alisema msimu huo walifika robo fainali ila msimu huu kama wakipambana zaidi wanaweza kufika mbali zaidi ya hapo.

"Malengo ya timu ni kuchukua ubingwa wa Afrika kwa maana hiyo tubapambana kadri ambavyo tunaweza kwa nyakati zote ili kufikia huko.

"Inaweza kutokea msimu huu tukafikia mafanikio yale au tukafika mbali zaidi," alisema Bocco, ambaye alizikosa mechi mbili za awali dhidi ya As Vita na Al Ahly kutokana majeraha.

Advertisement