Burnley yarejea Championship

Baada ya kupanda msimu huu na kukusanya pointi 24 katika mechi 37 za Ligi Kuu England, rasmi vijana wa Vincent Kompany, Burnley wameshuka daraja.
Burnley imeshuka daraja baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Tottenham kwa kichapo cha mabao 2-1 uliopigwa jana katika dimba la Tottenham Hotspur.
Katika mechi hiyo Burnley ilihitaji kuibuka na ushindi ili kuweka hai matumaini ya kubaki lakini kwa kipigo hicho hawatoweza kubakia hata wakishinda mchezo wao mmoja uliosalia.
Huu ulikuwa ni msimu wa tisa kwa Burnley kushiriki EPL, mara ya kwanza ikiwa ni 2009-10, ambapo ilipanda na kushuka kisha ikarudi tena msimu wa 2014-15 na ikashuka tena baada ya msimu mmoja.
Ikacheza Championship kwa msimu mmoja kisha ikarejea tena 2016-17, ikadumu katika EPL misimu michache kabla ya kushuka 2021-22 ambapo ilimaliza ya tatu kutoka mkiani.
Msimu uliopita ikamaliza bingwa wa Ligi ya Championship na kufanikiwa kupanda lakini imeshuka tena.
Hata hivyo, licha ya matokeo mabaya ambayo timu hii imeyapata msimu huu, matajiri wa Burnley wanaripotiwa kuwa na imani sana na kocha wao Kompany na wamepanga kuendelea naye akiwa aliipandisha daraja na ameshuka nayo.
Ushindi ambao Spurs iliupata katika mchezo huu uliwawezesha kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao, ikiwa inashika nafasi ya tano kwa pointi 63, huku Aston Villa iliyo nafasi ya nne ikiwa na pointi 67, hivyo kama Spurs ikichanga karata zake vizuri inaweza kuwashusha vijana hao wa Unai Emery katika mechi mbili zilizobaki