‘Chawa’ wajivunia kibarua chao

Sunday April 04 2021
Chawa pic
By Kelvin Kagambo

Cheo kinachobamba kwenye mitandao ya kijamii kwa sasa ni ‘chawa’, kama umepitwa ni kwamba, sasa hivi kuna watu wamejivunia umaarufu kwenye mitandao ya kijamii kwa kujipachika jina la chawa.

Jukumu lao kubwa ni kuwasifia watu wenye pesa au mastaa huku wakitarajia malipo kama vile pesa, ofa za bia na umaarufu.

Jina la chawa linatumika kwa sababu tabia ya watu hawa inafanana na mdudu chawa ambaye huishi mwilini mwa viumbe vingine huku wakifyonza damu zao kama chakula, yaani wanaishi kwa mtindo tegemezi.

Hata hivyo, huko kwenye mitandao ya kijamii kuna chawa ambao wamejivika jina hilo wao wenyewe huku wakionyesha kujivunia mno, wakiwamo Juma Lokole, msanii Baba Levo na mfanyabiashara wa saluni za kike anayefahamika kwa jina la Aristotee.

chawa pcc

Lakini pia kuna ambao wamevikwa jina hilo na wadau mitandaoni, hata hivyo wamegoma kukubali, akiwamo msanii H Baba na mtangazaji Burton Mwembe maarufu Mwijaku.

Advertisement

Mwananchi inakuletea mazungumzo na baadhi ya chawa maarufu wakifafanua maana ya chawa kwa mtazamo wao, pia wakiweka wazi namna wanavyoifaidika na je, kuna madhara ya kuwa chawa?


KUWA CHAWA NI NINI

Kwa mujibu wa msanii wa muziki Hamis Ramadhani maarufu H Baba, ambaye anatajwa kuwa chawa wa msanii Harmonize: “Chawa ni mtu anayejipendekeza kwa mtu mwenye pesa au maarufu ili anunuliwe vitu vidogovidogo au naye awe maarufu, ndiyo maana nakataa kuitwa chawa wa Harmonize,” anasema na kuongeza:

“Kwa hiyo kuniita chawa wa Harmonize ni makosa sana kwa sababu sijipendekezi kwake, siombi pesa wala sifuati umaarufu kwani nilikuwa maarufu kabla yake, isipokuwa ameonyesha heshima kwangu kama kaka yake, na mimi nimeamua kumuunga mkono,” anafafanua mkali huyo wa wimbo “Mpenzi Bubu”.

Kwa upande wa msanii Baba Levo ambaye anajivunia kuwa chawa wa msanii Diamond Platnumz na mwimbaji Shilole kiasi cha kujipachika jina la ‘Chawa Pro Max’, anasema maana ya chawa ni kuwa mtu unayeeneza sifa nzuri za mtu fulani mwenye pesa, kisha mwenyewe anakulipa kwa namna anayoona inafaa.

“Kwa mfano mimi kwa kuwa chawa wa Diamond tu amenilipia ada ya watoto wangu shule, ameninunulia gari ya zaidi ya Sh15milioni, kanilipa zaidi ya milioni 20 kwa ajili ya video ya wimbo wangu,” anatamba Baba Levo.


WANAVYOFAIDIKA

Wakati akijinadi aliyoyavuna kwa kuwa chawa, supastaa katika mtandao wa kijamii wa Instagram, Juma Lokole anasema kwa kuwa chawa wa msanii huyo, amepata ajira ya utangazaji wa Wasafi FM, kituo cha redio kinachomilikiwa na Diamond.

“Kwa sababu ukiwa chawa wa mtu maana yake unakuwa karibu naye, kwahiyo ukiwa karibu na mtu mzito kama Diamond anakupa michongo ili akuunge mkono na kukutia nguvu. Anaangalia unaweza kufanya nini anakusapoti huko,” anasema Juma Lokole na kuongeza kuwa anashauri watu wanaotaka kuwa chawa wahakikishe wanampigia tarumbeta mtu mwenye pesa kama Diamond.

“Ukiwa chawa wa mtu mwenye hela ya kununulia bia tu hakuna faida hapo. Kuwa chawa wa mtu ambaye anaweza kukupa mchongo mmoja tu ukabadilisha maisha yako.”

Chawa pccc

Kwa upande wake Aristote ambaye ni chawa wa mfanyabiashara maarufu wa maduka ya nguo anayefahamika kwa jina la Fred Vunja Bei pamoja na msanii Diamond, anasema yeye ni chawa mwenye akili na mara nyingi hapendi kupewa pesa kupitia kuwa chawa; na hapa anafafanua namna anavyofaidika.

“Bosi kama Diamond akinipa pesa sikatai, lakini mimi sio chawa wa kuomba omba pesa kwa sababu mimi sio mlemavu, nina mikono yangu na naweza kufanya kazi. Faida kubwa ninayoipata kuwa chawa wa Diamond ni umaarufu ambao unafanya inakuwa rahisi zaidi kufanya biashara zangu za saluni na nyinginezo,” anasema.


JE, HAWADHALILIKI?

Mtangazaji wa Clouds FM, Burtin Mwembe maarufu Mwijaku anayetajwa kuwa chawa wa Alikiba kwanza anakataa lakini pia anaweka wazi kuwa ni kujidhalilisha, hasa kwa mwanamume kujipendekeza kwa mwanamume mwingine kwa ajili ya kupata pesa ndogo ndogo.

“Naomba mimi msiniweke kwenye kundi la chawa, mimi sio chawa, nina elimu yangu kubwa na connection za kutosha, siwezi kuwa sina pesa mpaka kuanza kujipendekeza kwa wanaume wenzangu.

“Kuwa chawa ni kujidhalilisha sana, kwa mfano kuna chawa mmoja mwanamume, ana mke na watoto lakini aliwahi kusema kuwa kwa aliyofanyiwa na Diamond, angekuwa mwanamke angemzalia wanawake watatu. Mwanaume unaposema kauli kama hiyo unataka familia yako ikichukuliaje?” anahoji.

Kwa upande wake Aristote anasema yeye haoni kama ni kujidhalilisha ikiwa hakuna baya analolifanya zaidi ya kumsifia mtu anayempa madili.

“Najidhalilisha kivipi? Kwani kuna baya gani nimefanya. Mtu ananipa madili ya pesa kwa nini nimsilipe kwa kutangaza mema yake. Isititoshe wanaosema kuwa chawa ni kujidhalilisha ni wapiga domo tu kwenye mitandao, hawana lolote, hata pa kuishi.” anasema.

Advertisement