Huyu hapa mzee wa kama vipi "irudiwe"

Sunday May 23 2021
irudiwe pic
By Nasra Abdallah

Kuna usemi usemao Mungu akitaka kukupa, hakuandikii barua. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa mchekeshaji Oscar Mwanyanje, maarufu kwa jina la Mc Mboneke.

Msanii huyu amepata umaarufu mitandaoni kutokana na vichekesho vyake vya kujirekodi akiwa anakimbia huku usemi mkubwa ukiwa ni ‘samahani Serikali’, ‘Irudiwe’.

Mfano kuna clip yake imesambaa akisema: “Samahani Serikali vita ya majimaji wakati inapigwa, wengine tulikuwa hatujazaliwa, hivyo naomba irudiwe.”

Nyingine ni ile alipowasili Dar hivi karibuni na kupita katika daraja la juu pale Ubungo, na kusema anaomba ujenzi wa daraja hilo urudiwe kwa kuwa wakati linajengwa yeye hakuwepo.

Tayari vichekesho vyake hivyo vimepata umaarufu na watu mbalimbali kutumia maneno yake kujirekodi huku wakikimbia kama yeye.

Mwananchi imefanya naye mahojiano na kuzungumza mambo mbalimbali, ikiwemo kujua alipotokea hadi kujikuta maarufu.

Advertisement

Alipoanzia

Akiwa jijini Mbeya, alikuwa akifanya vichekesho vya majukwaani na hii ni baada ya kufanikiwa kupitia katika usaili wa kusaka vipaji uliokuwa ukiendeshwa na jukwaa la sanaa la ‘Kipaji Bidhaa’ la jijini humo.

Jukwaa hilo limekuwa likiwakusanya vijana wenye vipaji mbalimbali katika sanaa kwa ajili ya kuwatafutia fursa.

“Usaili ulifanyika mwaka jana, nashukuru kwa wachekeshaji mimi pekee ndio niliyepita, hivyo wakawa wananisimamia kazi zangu za sanaa mpaka hii leo ninavyozungumza na wewe,” anasema Mc Mboneke.

Ukiachilia mbali kazi hiyo ya sanaa, msanii huyu anasema anafanya pia biashara ya kuuza vitabu vya wanafunzi wa shule za awali.

Alivyowika mtandaoni

Mc Mboneke anasema anakumbuka ilikuwa mwanzoni mwa Mei mwaka huu, ambapo walikuwa kanisani kwao wakisherehekea ya siku ya vijana.

Anasema siku hiyo alikuwa amepiga suti yake kali ya bluu, ambapo kila alipopita watu walikuwa wakimtazama na kumsifia kuwa ametokelezea. “Hapohapo nikapata wazo, wakati nikiwa njiani narudi nyumbani kwa macho niliyokuwa nakodolewa na watu, nikajirekodi clip na kusema samahani Serikali, jamani sisi watu tunaovaa suti tafadhali tuwe tunapewa ulinzi mkali vibaka wasije wakatuvamia,” anaeleza.

Clip hiyo anasema bila kutarajia aliiona inasambaa ambapo watu ndio walikuwa wakimwambia wamemuona: “Wakati mwingine nakuwa sina bando, nikawa nakopa ili ninunue nijione au naangalia kwenye simu za wenzangu waliokuwa na bando,” anasema.

“Kuanzia hapo nikagundua kuna fursa mitandaoni, nikawa najirekodi viclip na kuvirusha, ndiyo nikawa maarufu naitwa kama hivi kuhojiwa na vyombo mbalimbali vya habari na watu kuniiga huko mitandaoni namna ninavyoongea, kitu ambacho kwangu mimi ni hatua kubwa ukijumlisha msoto niliosota katika sanaa,” anasema.

Ujio wake Dar na mapokezi

Mc Mboneke anasema alikwenda Dar wiki iliyopita baada ya meneja wake kumtaka afanye hivyo kutokana na watu kutaka kuonana naye.

Hata hivyo, anasema mapokezi yake yamekuwa tofauti na alivyodhani, ambapo amepokelewa kwa ukarimu mkubwa.

Pia anasema akiwa na siku chache katika jiji hilo la kibiashara ameweza kupata michongo mbalimbali, ikiwemo ya kupata matangazo na kuwa balozi wa huduma na bidhaa mbalimbali.

“Jambo hili linanifanya nifikirie kuhamia Dar kwa kuwa naona kama kipaji changu kimeeleweka zaidi, kwani Mbeya ni kwetu lakini bado hawajaelewa kabisa sanaa ya uchekeshaji jukwaani, wakati mwingine unaweza kujikuta unajichekesha mwenyewe.”

Wito

Msanii huyu anatoa wito kwa jamii kuwathamini wachekeshaji, kwani mbali ya kuchekesha, pia ni watoaji elimu wazuri.

Mc Mboneke amewaomba wasanii wenzake kuungana mkono, hususan kwao chipukizi kama yeye ambao wanahitaji kujua njia za kupita kufikia mafanikio.

Anavutiwa na nani?

Anawataja wasanii wanaomvutia na kuwachukulia kama mifano kuwa ni Pembe, Senga na Joti.

Mboneke amezaliwa Jijini Mbeya miaka 23 iliyopita, amesoma Shule ya Msingi Sistila ambapo alimaliza mwaka 2011, na kisha kujiunga na Shule ya Sekondari hapohapo kabla ya kwenda kidato cha tano na sita Shule ya kutwa Mbeya na kumaliza mwaka 2018. Kutokana na kukosa mkopo wa kwenda chuo kikuu, ndio akaamua kujishughulisha na kazi ya kuuza vitabu na uchekeshaji, kazi anayoifanya hadi sasa.

Advertisement