Mauaji ya rapa AKA yanavyohusishwa na kisasi kifo cha Anele

Msanii wa Hip Hop wa Afrika Kusini, Kiernan Jarryd Forbes ‘AKA’ alipumzishwa jana Februari 18, 2023 katika makazi yake ya milele baada ya kuuawa usiku wa Februari 10 kwa kupigwa risasi huko Durban nchini humo.

Video za CCTV zimeonyesha AKA baada ya kuwasili katika club ya muziki, Yugo ambapo inadaiwa angetumbuiza, mtu mmoja alijitokeza na kumuua kisha kutokomea.

AKA, 35, kipindi cha uhai wake aliwahi kuja Tanzania mara kadhaa na kufanya kazi na baadhi ya wasanii kama Diamond Platnumz na Joh Makini ambapo waliachia vibao kama ‘Make Me Sing’ na ‘Don’t Bother’.

Kufuatia kifo chake kumekuwa na hisia mseto miongoni mwa mashabiki iwapo mauaji hayo yalipangwa kwa lengo la kulipiza kisasi, madai ambayo hayajathibitishwa na mamlaka husika hadi sasa.

Aprili 2021 aliyekuwa mpenzi wa AKA, Anele Tembe, 22, alifariki katika mazingira ya kutatanisha, ripoti zilieleza kuwa alijirusha kutoka ghorofa ya 10 hadi chini katika hoteli moja huko Cape Town.

Hata hivyo, baba mzazi wa Anele, Moses Tembe ambaye ni mfanyabiashara maarufu Afrika Kusini alikanusha madai ya binti yake kujiua katika siku ya mazishi yake, akidai kuwa mtoto wake hawezi kujiua kama ambavyo iliripotiwa.

Moses alikuwa anashuku kuwa AKA alimuua binti yake kwa bahati mbaya au makusudi, hivyo ili kupoteza ushahidi alichukua uamuzi wa kumtupa chini kutoka ghorofani.

Katika mitandaoni ya kijamii kulisambaa video ikonyesha AKA akigombana na Anele, lakini AKA alikanusha madai kuwa ugomvi wa kimapenzi ulisababisha kumuua mpenzi wake huyo, huku waendesha mashtaka akiitupilia mbali kesi hiyo. Kwa kipindi chote AKA alijitambulisha kama mtu asiye na hatia kuhusu kifo cha Anele, hadi kutoa wimbo wa maombolezo ‘Tears Run Dry’ hapo Oktoba 2021. Kuna madai kuwa eneo alilouawa AKA, Durban ndipo anaishi baba mzazi wa Anele, Moses Tembe, ndiyo maana wanaunganisha matukio hayo na kuibua swali. Je, kifo cha AKA ni kisasi?. Katika hatua nyingine, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amekataa ombi lililotolewa na Mkuu wa jimbo la Gauteng, Panyaza Lesufi aliyeomba AKA afanyiwe mazishi ya kitaifa ambapo jeneza lake lifunikwe na bendera ya taifa na bendera kupeperushwa nusu mlingoti kutokana mchango wake katika jamii,. Tayari familia ya AKA imeweka wazi kuwa albamu ya Rapa huyo, ‘Mass Country’ itaachiwa kwa lengo la kuheshimisha alichokifanya na isitoshe aliwekeza nguvu na jitihada kubwa kuiandaa, huku wimbo wake, ‘Company’ alioshirikiana na Kiddominant ukiachiwa jana, Ijumaa.