'Pele' achana na soka, muziki na filamu nako moto

Mfalme wa soka duniani, Pele alipenda sana   muziki na amekuwa mwigizaji wa filamu.

Jina lake halisi  ni Edson Arantes do Nascimento, lakini alipewa jina la utani la Pele baada ya kushindwa kutamka vizuri jina la Bile aliyecheza mpira na baba yake.

Pele katika mapenzi yake kwenye muziki pia amekuwa mtunzi wa nyimbo, lakini hakutaka sana kuonyesha mapenzi yake ya muzuki hadharani akitaja sababu kadhaa.

“Sitaki watu waanze kulinganisha Pele mtunzi wa muziki na mchezaji wa soka. Hiyo itakuwa na haki kubwa kwa sababu kwenye soka kipaji changu ni zawadi kutoka kwa Mungu, muziki ni suala la kujifurahisha,” alinukuliwa akisema Pele.

Hata hivyo, siku tatu kabla ya kuazimisha kumbukumbu ya kutimiza miaka 80 ya kuzaliwa, Pele alitoa singo aliyokuwa ameitunga ikiitwa ‘Acredita No Véio’ au Listen To The Old Man (msikilize mzee).

Wimbo huo Pele aliuimba na Rodrigo  Gabriela ambaye ni mshindi wa tuzo ya Grammy mwaka 2019, “Sisi sote ni mashabiki wa soka,” alisema Rodrigo Gabriela aliyekulia katika jiji la Mexico.

“Tuna habari nyingi kuhusu Pele, lijendari wa Brazil aliyeipatia ushindi wa Kombe la Dunia nchi yake mwaka 1970 kwenye ardhi ya nchi yetu,” alisema Gabriela.

Alisema Pele ni mchezaji gwiji wa soka kwa muda wote, lakini pia ana kipaji cha utunzi na uandishi wa mashairi ya muziki. “Ni heshima kwetu kufanya kolabo na Pele katika tukio la kutimiza umri wa miaka 80,” alisema.

Singo ya ‘Acredita No Véio’ iiandikwa na Pele mwaka 2005 akishirikiana na mwanamuziki wa Jazz wa Brazil, Ruria Duprat, ambaye ni maarufu kwa kupiga muziki wa Jazz na mastaa kama Diana Krall, Randy Brecker na Ron Carter. “Nilitunga muziki huu kwa kuwa wakati nikichezea timu ya Santos kocha mara kadhaa alikuwa akisema tukifungwa hayo ni makosa ya wachezaji, lakini  tukishinda ni miujiza au nguvu ya giza, ‘macumba.’

“Wimbo ulikuwa ukitania kuhusu hali hiyo, kiukweli ‘macumba’ haisababishi kushinda mchezo,” alisema Pele.
Kuna wakati Pele alinukuliwa akisema: “Nimeandika vitabu vingi, nimefunga magoli mengi, ni baba wa watoto, nimepanda miti mingi. Kitu pekee cha kukumbukwa kinachokesekana kwenye maisha yangu ni muziki.”

Hata hivyo, Pele katika maisha yake hakujiweka mbali na muziki na hasa gitaa alilokuwa akilicharaza akiwa kwenye mapumziko kujiliwaza. “Hakuwa mbali na gitaa na alibeba rekoda kurekodi tyuni alizokuwa akipiga,” aliandika Lawrie Mifflin kwenye kumbukumbu ya Pele kwenye gazeti la New York Times.

Pia, Pele alitoa singo na albamu nyingi kwa kufanya kolabo na mtunzi wa muziki wa Brazil Sérgio Mendes waliotunga wimbo ukiitwa ‘Sergio Mendes’ Pelé.’
Sérgio Mendes pia alikuwa mtaalamu wa sauti wa ‘documentary’ ya maisha ya Pele kwenye soka, uimbaji na utunzi wa nyimbo za muziki.

Pele aliwahi kutumbuiza nyimbo mbili kati ya nyimbo zake nyingi ambazo ni “Meu Mundo É uma Bola (My World Is a Ball) ‘yaani duniani yangu ni mpira’ na “Cidade Grande (Big City)” yaani ‘Jiji Kuu’, akishirikiana na mwimbaji wa Brazili Gracinha Leporace. Pia, Pele aliwahi kutunga wimbo unaosema “Esperança” kwa ajili ya ufunguzi wa mashindano ya Olympic yaliyofanyika Rio de Janeiro mwaka 2016.
Wimbo huo wa kwaya ulihusu vijana na uliimbwa na watoto wa kwaya ikichanganywa picha ya Pele akiwa studio na baadhi ya vijana wakicheza soka.

Mwaka 2014 alitoa albamu iliyoitwa ‘Pelé Ginga’ akifanya kolabo na wanamuziki wakubwa wa  Brazil Gilberto Gil, on “Quem Sou Eu”, na Elis Regina, on “Perdão Não Tem” na  “Vexamão”.
Albamu hiyo  ilikuwa na kipengele cha ‘Rappin’ Hood in “Ginga”, maneno yaliyokuwa yakielezea uchezaji soka wa Brazil na namna ya kumiliki mpira.

Nyimbo kuhusu Pele
“Pele na Pele” ni wimbo ulioimbwa nchini Brazil uliotoka Julai 2, 2022 kwenye Chaneli ya “Gaab Oficial” ikiwa ni video ya muziki inayojulikana sana ambayo ilichukua nafasi katika chati maarufu kuwa nyimbo bora nchini humo ukiwa na mashairi:  “Kumtazama akicheza ilikuwa kutazama furaha ya mtoto pamoja na neema ya ajabu ya mwanamume.”

Wimbo mwingine uliitwa ‘Kama Pele’ ni wimbo uliopata mafanikio katika chati zote za muziki kwa mara ya kwanza ulitoka Septemba 29, 2021.

Pele kwenye Filamu
Sehemu nyingine isiyojulikana sana ya Pele ni eneo la uigizaji ambapo katika maisha yake amekuwa mwigizaji wa filamu 10, mojawapo akiwa na Sylvester Stallone na Michael Caine.
Kwenye Mtandao wa Data ya Filamu ya Mtandao, IMDB, ambayo inarekodi mienendo yote ya ulimwengu wa sinema, Pele anaonekana kama mwigizaji katika maonyesho ya sinema.

Filamu maarufu ya Pele ni inayohusu “ukwepaji au ushindi” iliyoigizwa Hispania au kwa jina lingine “Kutoroka kwa ushindi” huko Amerika Kusini) na ilitoka mwaka 1981.

Mwongozaji wa filamu hiyo alikuwa John Huston (mkurugenzi anayekumbukwa wa “The Maltese Falcon”), washiriki wengine wakiwa Sylvester Stallone na Michael Caine.

Haijulikani ikiwa Huston alivutiwa na uigizaji wa Pele, ambaye pia alionekana kinyume chake katika filamu ya 1983 “A Minor Miracle”, ambapo aliigiza mwenyewe.

Historia
Pele ambaye Oktoba 23, 2022 alisherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa kutimiza umri wa miaka 82, juzi Desemba 29, 2022 alifariki dunia kwa maradhi ya kansa na figo.

Septemba 2021 Pele alifanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye utumbo wake katika Hospitali ya Albert Einstein mjini Sao Paulo. Kabla ya kurejeshwa hospitalini mwishoni mwa Novemba. Pele, alikua nyota wa soka wa kimataifa akicheza fainali za Kombe la Dunia akiwa mchezaji pekee mwenye umri mdogo wa miaka 17, alipoisaidia Brazil kushinda Kombe la Dunia mwaka 1958.

Mchezaji pekee aliyeshinda Kombe la Dunia mara tatu, akinyakua taji hilo 1958, 1962 na 1970, Pele alitangazwa kuwa mchezaji bora wa Karne wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mwaka 2000.

Chapa ya kimataifa
Pia, jina la Pele linatambulika katika nchi zote duniani, ni chapa ya kimataifa kwa wapenda soka na hata wasiopenda soka. Kwa Tanzania mtu akifanya vizuri aliaambiwa “umecheza kama Pele.” Kuna wakati Pele mwenyewe alitania kuwa kulikuwa na chapa tatu tu za kimataifa: Yesu, Coca Cola na Pele.

Balozi
Mwaka 1992, Pele aliteuliwa kuwa balozi wa Umoja wa Mataifa wa ikolojia na mazingira, baadaye akafanywa kuwa balozi mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (Unesco) , pia Kamanda wa heshima wa Dola ya Uingereza.

Hazina ya Taifa
Serikali ya Brazil ilimfanya Pele kuwa Hazina ya Taifa baada ya vilabu tajiri duniani zikiwemo Manchester United na Real Madrid kujaribu kumsajili mwanasoka huyo. Serikali ya Brazil ilimtangaza

“Hazina ya Taifa” ili kumzuia kuhamishwa, kwa maana ya kwenda kucheza nje ya nchi hiyo.
Nyongeza na Peter Akaro