Sugu alivyosafisha njia kwa Jide, Afande Sele

Sunday June 19 2022
sugu pic
By Mwandishi Wetu

Kuna sentensi tamu tatu tofauti. The Autobiography. Muziki na Maisha. From The Street To Parliament. Hizi zipo juu ya jalada (‘kava’), la kitabu cha Joseph Osmund Mbilinyi, maarufu kama Sugu aliyekuwa mbunge wa Mbeya Mjini kwa vipindi viwili tofauti.

Sugu alipewa kura za kumiliki jimbo hilo kwa mara ya kwanza mwaka 2010, kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Ushawishi wa John Mnyika, ulimfanya mkongwe huyu wa muziki wa kizazi kipya aachane na mipango mingine mingi na kujikitika katika siasa.
Kabla ya kuingia kwenye ‘mchezo’ wa siasa, Sugu alifanya kila kitu katika maisha na kwenye muziki wake.

Ni kama hakuna alilobakiza, aliudai muziki kuliko muziki unavyomdai yeye.
Ukiachana na wingi wa ‘shoo’ ndani na nje ya nchi, albamu zaidi ya 10 mpaka kufikia mwaka 2010, lakini Sugu alikuwa mmoja wa wabongo wachache wenye kitabu cha maisha yake.

Kitabu hiki ambacho tunachambua baadhi ya kurasa zake, kinaongelea maisha yake tangu alipozaliwa na misele yake yote kwa jumla. Ni kitabu kitamu na kitamu ‘elimika’ kwa kila rika. Kinaeleza maisha ya mmoja kati ya wasanii wa ‘hiphop’ wa awali Bongo, aliyeshiriki kikamilifu kuueneza na kuukuza muziki huu na baadaye kugeuka biashara kubwa hivi sasa.
Katika kitabu hiki, Sugu anasema yeye ni miongoni mwa watu wale wa kwanza kabisa waliochana kwa lugha ya Kiswahili na kuichana Serikali bila kificho.

Hapo kabla wengi walitumia Kiingereza.
Anakiri wapo waliofanya muziki huu kabla, lakini hawakuchana Kiswahili, bali Kiingereza wakiiga wasanii wa nje.

Advertisement

‘Kuchana’ Kiswahili kulimfanya awe tofauti na hata kupendwa zaidi.
Sugu anasema hakufika alipokuwa (kwa wakati ule), kwa bahati au kwa upendeleo kama wengi wanavyofikiri, badala yake anasema alisota sana mpaka kufikia hatua ya kuitwa Sugu kama ilivyo sasa!
Mwamba anadai kapitia mengi sana. Kama ‘uhuni’ ule wakati akisoma Mbeya Day. ‘Uhuni’ uliofanya atimuliwe shule akiwa kidato cha tatu na kuhamia Mtwara.
Baada ya kumaliza shule na baba yake akiwa katangulia mbele ya haki, ugumu wa maisha na mzigo mzito alioachiwa wa kumtunza mama na kuhakikisha wadogo zake wote wanasoma ulifanya Sugu apige moyo konde.

Na akataka kwenda ‘Sauzi’ kusaka maisha, kama ‘masela’ wengi wa wakati huo walivyofanya, lakini bado hakufanikiwa na safari yake iliishia katika ardhi ya Robert Mugabe.
Ndoto zake za kusafiri kusaka maisha ng’ambo, zilikuja kuwa kweli akiwa tayari ni staa wa muziki.

Ulaya alikwenda mara nyingi kusaka maisha na sio ‘Sauzi’ tena, lakini nako bado hakuweza kutoboa.
Mara zote mwamba alipokwenda nje ya nchi, alikutana na changamoto kama za kufungwa mipaka au kuumwa.

Kitu hiki kilisababisha mara zote arudi nyumbani na zaidi akimkumbuka mama yake.
Katika hili tunajifunza kitu, kwamba hadithi za ukienda Ulaya utatoboa haraka, zinavutia sana.

Kama ukienda mwenyewe ukaone hayo maisha yao mazuri, ndipo unaona ukweli halisi mwenyewe.
Pia katika kitabu, Sugu anatuonyesha nguvu ya watu wanaokuzunguka wanaweza kukufanya uinuke haraka au uanguke. Na hili utaliona kwenye maisha yake kupitia kitabu hiki tangu utotoni mpaka ukubwani.
Ni rafiki waliofanya awe mhuni shule, waliomfundisha kuandika mashairi kwa Kiswahili, badala ya Kiingereza.

Ni marafiki waliompa ‘konekisheni’ na watu muhimu kwa wakati huo.
Na ni rafiki waliomzunguka wakati huo walitengeneza njama za kumwangusha au kumpoteza na kusababisha atangaze kustaafu muziki bila kutaka. Ni vyema kutengeneza marafiki sahihi.
Sugu pia, anatupa elimu ya wazazi jinsi walivyo na nafasi kwenye maisha ya watoto wao.

Anamkubali sana baba yake kwa mengi aliyoyafanya, kikubwa ni kutafuta maisha na kuitunza familia yao vizuri.
Pia, amemuelezea mama kama mtu aliyetoa mchango mkubwa kwenye muziki wake, alimruhusu aingie kwenye gemu ya muziki miaka hiyo ambayo muziki ulionekana ni kitu cha hovyo, wazazi wengi ilikuwa vigumu kuwaruhusu watoto wao wawe wanamuziki.

Lakini mama yake Sugu ilikuwa tofauti na akawa mbele ya wakati, akaruhusu mtoto wake wa kwanza kufanya muziki.
Anatueleza kuwa mama yake, Desderia Mbilinyi ndiye aliyekuja kuwa mhimili mkubwa pale alipotaka kuacha muziki, kwa kuwa miaka 1990, alimpa moyo akimtaka aendelee na muziki wake.
Pamoja na mengine, ndani ya kitabu hiki Sugu anatueleza alivyojenga historia ya kuwatoa wasanii wawili, Lady Jaydee na Afande Sele, aliowapa nafasi kwenye albamu yake ya tano ya Milenia.
Albamu hii aliitoa mwaka 2000.

Ndani yake yupo Afande Sele kwenye wimbo ‘Nikianguka’ na Jaydee akipewa mchongo kwenye kiitikio cha ngoma “Mambo ya fedha”. Hii ilikuwa kubwa sana.
Lakini kabla ya kuwapa nafasi hizi, hawa wote wawili kuna vitu vingi nyuma ya pazia na ukisoma kitabu hiki utajifunza zaidi. Afande Sele alifika mjengoni kuomba msaada wa kutolewa kimuziki.
Imani ya Sugu kwa Afande, ilifanya ampeleke kwa Master Jay Osterbay ili aingize sauti kwenye moja ya nyimbo za Sugu.

Kumbuka Sugu wa wakati huo alikuwa hafikiwi kirahisi sana na ukipewa shavu lake imetoka hiyo.
Mara ya kwanza Afande Sele kuingia chumba cha kuingizia sauti alikosa nguvu na kukaa chini na kushindwa kuendelea (hofu). Mara yake ya kwanza kufika kwa Master Jay. Mara yake ya kwanza kuingia studio. Anaingiza sauti kwenye wimbo wa msanii mkubwa Afrika Mashariki.

Kifupi akitoka hapo naye anakuwa sehemu ya wasanii maarufu. Lazima hofu itawale na nguvu za magotini zitoweke.
Sugu akalazimika kuingia studio tena. Na kumshikilia Afande Sele ili aweze kusimama na kuingiza sauti.

Kuna imani kubwa ndani ya moyo wa Sugu, iliyoamini katika Afande Sele.
Baada ya Sugu kufanya hilo, Afande akaweza kuingiza ‘vesi’ ya ngoma ya “Nikianguka”. Kuanzia hapo akawa mtu mbele ya mashabiki na kupata nafasi kubwa kwenye albamu ya “Muziki na Maisha”.
Lady Jaydee pia haikuwa rahisi mwanzo. Kabla ya kufanya naye ngoma ya “Mambo ya Fedha”. Ruge (RIP) alikuwa akiomba Sugu apande jukwaani Jaydee akiwa anaimba ili apate shangwe.
Wakati ule uso wa Sugu ukitokea tu jukwaani, mashabiki walilipuka kwa shangwe. Ruge akatumia nafasi hiyo kumjenga Jaydee. Mwaka mmoja baadaye akatoka na albamu yake ya “Machozi” na kuwa historia mpaka leo.
Mbali ya Jide na Afande, Sugu pia amewahi kuwasaidia wasanii kama Soggy Doggy na GWM, baada ya kuwagomea ‘Wadosi’ kutoa albamu yake kwanza mpaka watoe albamu ya Soggy Doggy pamoja na ile ya GWM. Kuna wasanii walikuwa na albamu lakini ‘Wadosi’ hawakuwaamini kama wanaweza kuuza.

Kitu hicho kilikuwa kinamkwaza Sugu, ndipo akaamua kugoma kutoa albamu zake mpaka kwanza ‘Wadosi’ wakakubali kutoa albamu za wengine.
Hapo ndipo Soggy Doggy na GWM walipopata mchongo kwa ‘Wadosi’. Kifupi Sugu alikuwa anataka haki kwa wasanii hata kabla yeye hajaanza kupata haki stahili. Hiki anachosimamia leo kasimamia miaka mingi nyuma.

Advertisement