Ushahidi wamuweka pabaya R Kelly

Friday September 24 2021
ushahidipic
By Mwandishi Wetu

New York, Marekani (AFP). Mwimbaji wa R&B, R Kelly alitumia "uongo, ujanja, vitisho na nguvu" kuendesha "genge" lililomuwezesha kufanya uhalifu wa kingono kwa miaka takriban 30, waendesha mashtaka walisema Jumatano katika majumuisho ya hoja zao za kesi ya tuhuma za ubakaji .

Katika kutoa hoja zao kuelekea mwisho wa kesi hiyo, mwanasheria msaidizi wa serikali ya Marekani, Elizabeth Geddes alitumia saa mbili za mwanzo kufanya majumuisho hayo, akiiambia mahakama kuwa Kelly, ambaye alitamba duniani katika muziki wa R&B, "alitumia fedha na jina lake kuficha uhalifu."

R Kelly, ambaye jina lake halisi ni Robert Sylvester Kelly, aliiteka dunia kutokana na nyimbo zake kama "I Believe I Can Fly", "Bump N' Grind", "Your Body's Callin'", "Gotham City", "Ignition (Remix)", na "The World's Greatest" katika miaka ya tisini, kiasi cha kuitwa "Mfalme wa R&B".

Lakini Februari 22, 2019, Kelly alishtakiwa kwa makosa kumi ya uhalifu wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana wadogo.

Serikali ilikuwa na kazi ya kuthibitisha kuwa mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 54 aliendesha genge la marafiki wahalifu ambao walifanikisha vitendo vyake vya kunyanyasa wanawake, kunajisi watoto, ikitumia waathirika waliotoa ushahidi kwa wiki sita, kuwa msanii huyo aliwadhuru kingono, kimwili na kiakili.

"Bila ya wao kumsaidia, mshtakiwa asingeweza kufanya uhalifu wa aina hiyo kwa karibu miongo mitatu," Geddes aliiambia mahakama, akiwa amesimama mbele ya bango linaloonyesha picha za watu wa genge hilo zinazozunguka sura ya Kelly.

Advertisement

Mwendesha mashtaka alisema wafanyakazi wake na watu waliomzunguka walifanya vitendo vya kihalifu wenyewe au "kuvifanikisha" wakati "hawakuuliza maswali" na "walitekeleza kwa ufanisi amri za mshtakiwa."

"Walikuwa ni njia ya kufanikisha vitendo vyake vya kihalifu," alisema Geddes.

Soma zaidi: R Kelly amwaga chozi akihojiwa, miaka 70 jela inamsubiri

Majumuisho hayo ya upande wa serikali yamekuja baada ya wiki tatu za kumhoji na ushuhuda wa utetezi wa mwimbaji huo, ambaye aliita mashahidi watano, akiwemo mfanyakazi wake wa zamani na rafiki wa tangu utotoni ambaye alisema binafsi hakuona vitendo hivyo vya kutisha vya Kelly.

Hatua hiyo ya ushahidi ilikuja zaidi ya mwezi mmoja wa kutoa vielelezo kwa kutumia michoro iliyowasilishwa na waendesha mashtaka.

Kukiwa na mashuhuda 45 wakiwemo 11 wanaotuhumu -- tisa wanawake na wawili wanaume -- wanasheria wa serikali walipambana kuthibitisha vitendo hivyo vya R.Kelly na washirika wake.

Wanawake walisema walibakwa, kupigwa, kuleweshwa kwa dawa, kushikiliwa na hata kunyimwa chakula au kwenda bafuni.

Sita kati ya watu waliothirika walikuwa watoto wakati Kelly alipoanza mapenzi nao. Waathirika wengi pia walisema mara kwa mara mwimbaji huyo alichukua picha za video za matukio hayo, kitu ambacho ni kosa inapofikia watoto kuhusishwa.

Mwanamke mmoja alisema Kelly alimlazimisha atoe mimba wakati alipokuwa na umri chini ya miaka 20. Wanne walisema waliambukizwa malengelenge (herpes) baada ya kufanya mapenzi na mwanamuziki huyo, ambaye walisema hakuwaambia kuwa ana ugonjwa wa virusi hivyo usiotibika.

Mashtaka yanahusu zaidi wanawake sita: Jerhonda, Stephanie, Faith, Sonja na mwanamke ambaye alitoa ushahidi kwa kutumia jina bandia, pamoja na nyota wa zamani wa muziki wa R&B, Aaliyah, ambaye alifariki katika ajali ya ndege mwaka 2001, lakini Kelly alimuoa kinyume cha sheria wakati akiwa na miaka 15.Advertisement