Aisee! Diamond hapoi, haboi...

Sunday November 07 2021
diamond pic
By Peter Akaro

Huenda mwimbaji wa Bongofleva kutoka WCB Wasafi, Diamond akaufunga mwaka huu kwa kishindo cha aina yake kwa sababu hadi sasa amependekezwa kuwania tuzo 18 za kimataifa.

Mwaka huu Diamond alikuwa msanii pekee ukanda wa Afrika Mashariki kutajwa kuwania tuzo za BET 2021 katika kipengele cha Best International Act, ikiwa ni mara yake ya tatu.

Tuzo hizo kubwa duniani ambazo zilitolewa Juni 28, 2021 huko Los Angeles, Marekani, hazikumpa raha, kwani ushindi ulikwenda kwa Burna Boy wa Nigeria, ambaye aliandikisha ushindi wake wa tatu mfululizo.

Hata hivyo, hivi karibuni Diamond alifanikiwa kushinda tuzo ya msanii bora wa mwaka Afrika kutoka Ghana Music Awards UK, baada ya kuwabagwa wakali wengine kama Burna Boy, Davido, Wizkid, Master KG na Patoranking.

Kwa sasa Diamond anazichanga karata zake vilivyo katika tuzo nne za kimataifa ambazo anawania vipengele 18, akiwa ndiye msanii pekee kutoka Tanzania na Afrika Mashariki kufikia idadi hiyo.

Diamond amechaguliwa kuwani tuzo za MTV Europe Music Awards (MTV EMA) 2021 katika kipengele cha Best African Act, washindani wake ni Wizkid (Nigeria), Tems (Nigeria), Amaarae (Ghana) na Focalistic (Afrika Kusini).

Advertisement

Katika tuzo za All African Music Awards (AFRIMA) ambazo zinatarajiwa kutolewa mwezi huu nchini Nigeria, Diamond amechaguliwa kuwania vipengele saba kufuatia kufanya vizuri zaidi na wimbo ‘Waah’ ambao kamshirikisha Koffi Olomide kutoka DR Congo.

Miongoni mwa vipengele anavyowania ni Best Male Artiste In Eastern Africa, Artiste Of The Year, Best African Collaboration, Best African Video, Song of The Year na Best Artiste, Due or Group in African Dance or Choreography

Upande wa tuzo za African Entertainment Awards USA (AEAUSA) kutoka Marekani kateuliwa kuwania vipengele vitano ambavyo ni Best Male Artist, Best Collaboration, Artist of The Year, Best Music Video na Song of The Year.

Kwenye tuzo za African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) kutoka Marekani pia, hapa anawania vipengele vitano ambavyo ni Best Male East Africa, Artist of The Year, Best Live Act, Best Collaboration na Afrimma video of the Year.

Tuzo zote anazowania ameshawahi kuzishinda kwa nyakati tofauti na mshindi anapatikana kwa kupigiwa kura na mashabiki, tofauti na ilivyokuwa upande wa BET.

Utakumbuka Diamond anashikilia rekodi ya kushinda tuzo saba za Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) zilizotolewa mwaka 2014 kwa usiku mmoja, anakaribiwa na Alikiba aliyeshinda tuzo tano mwaka 2015, ikiwa ni sawa na 20 Percent kwa mwaka 2011. Kwa kipindi cha miaka 12 katika muziki wa Bongofleva, Diamond ameshinda na kutunukiwa tuzo zaidi ya 46 za ndani na za kimataifa, huku akimpiku Lady Jaydee wenye tuzo zaidi ya 35 katika kabati lake.

Hata hivyo mtayarishaji mkongwe wa muziki nchini, Master Jay anasema tuzo nyingi za kimataifa hazina mchango wowote wa kuikuza Bongofleva.

“Haziongezi mauzo, zinasaidia nini? labda BET, ila hizi nyingine ambazo zinatengenezwa na watu wa Afrika kwa sisi ambao tunajua kiundani tunaona ni ujanja ujanja tu.Lakini ukiangalia platform kubwa mfano BET kule msanii ahitaji kwenda kushinda, kutajwa tu ni heshima tosha, hizi nyingine ni watu tu wanapiga fedha hakuna cha maana kinachoendelea”anasema Master Jay ambaye ametayarisha muziki kwa zaidi ya miaka 20 ndani ya MJ Recods.


Historia ya tuzo

Tuzo za AEAUSA zilianza kutolewa Oktoba 2015 huko New Jersey, Marekani zikiwa na vipengele 30.

Huku za AFRIMA zilianza Desemba 2014 huko Nigeria zikiwa na jumla ya vipengele 37, waandaji wanashirikiana na Umoja wa Afrika (AU), lengo likiwa ni kuutangaza na kuupa thamani muziki wa bara hilo. Pia tuzo za AFRIMMA zilianza Julai 2014 Texas, Marekani kwa ajili ya kuwatunza wasanii, watangazaji, Djs na wadau wa burudani.

Akizungumzia tuzo hizo mmoja wa Meneja wa Diamond, Said Fella, maarufu Mkubwa Fella anasema, “Tuzo kwa msanii yoyote ni kipimo cha kukubalika au utokubalika kazi yake, pia inampa fursa ya kufurahia, kujivunia alichokifanya.

“Kwetu sisi Diamond kuingia au kutajwa katika tuzo achilia mbali kushinda ni ushindi kwake na kwetu kama lebo, pia inampa nafasi ya kuzidi kujulikana kwa sababu tayari anajulikana, pia inamfungulia fursa za nyingi zinazohusiana na kazi zake”anasema Fella.

Advertisement