Alichokisema Rais Samia baada ya kumpigia simu Nandy

Sunday June 27 2021
nandypic
By Peter Akaro

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amempigia simu msanii Nandy wakati akiwa jukwaani akiwatumbuiza wakazi wa Dodoma.

Nandy kupitia tamasha lake la Nandy Festival jana Jumamosi Juni 26, 2021 alikuwa mkoani Dodoma ikiwa ni baada ya kufanya tamasha hilo mkoani Mwanza na Kigoma.

Nandy anayetamba na nyimbo kadhaa ikiwemo Nimekuzoea alipanda jukwaani akiwa na simu mkononi na kuwaeleza mashabiki wake kuwa Rais Samia anataka kuongea nao.

Kupitia simu hiyo, kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema anashukuru tamasha hilo kufanyika siku ambayo anatimiza siku 100 tangu alipoapishwa Machi 19, 2021.


"Nina majukumu ya kizazi Dar es Salaam lakini ningekuwepo hapo siku ya leo (jana). Nami nawashukuru leo nikitimiza siku ya 100 mko Dodoma mkitumbuiza vijana, waambie ninawapenda sana,” amesema Rais Samia.

Advertisement


Kwa upande wake Nandy amemshukuru Rais Samia kwa kuonyesha upendo na kumueleza kuwa hakutegemea kama angetumia siku ya ke ya 100 katika uongozi kusherehekea nao. 


"Ni kitu kikubwa katika harakati ambayo naifanya katika Nandy Festival, nikiwa kama binti na yeye akiwa kama Mama, imenitia nguvu kama mtoto kwa hiki ninachokifanya. Mama anaona kila hatua ambayo vijana wake tunafanya, niseme tu ninaahidi kufanya kazi kwa bidii na kuwa mfano kwa mabinti na vizazi vijavyo," amesema Nandy.


Baada ya Dodoma Nandy Festival ambayo imekuwa ikifanyika toka mwaka 2017 ataelekea mkoani Arusha. Nandy ni msanii mwingine wa Bongofleva ambaye tamasha lake limekuwa na mwendelezo na mafanikio baada ya Diamond Platnumz mwenye Wasafi Festival.Advertisement