Alikiba: Kuna watu wanakopi video za watu, kupitia ‘Salute’ nimewafundisha kitu kipya

Thursday July 01 2021
alikibapic
By Peter Akaro

Msanii wa Bongofleva, Alikiba amesema video ya wimbo 'Salute' anaonekana kuvalia kijeshi haijatumia gharama kubwa licha kutaka kufanya kitu tofauti.

Amesema  wasanii wengi sasa wamekuwa na tabia ya kukopi video za wenzao jambo ambalo ameona asilipe nafasi kwenye muziki wake.

Alikiba amesema wazo la kufanya hivyo lilichochewa na Rubeboy wa Nigeria aliyemshirikisha katika wimbo huo, lakini pia amefanya hivyo kama kutoa heshima kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kazi nzuri wanayofanya.

"Tulikata watu waone tunataka kufanya kitu cha tofauti kwa sababu idea zipo nyingi sana, watu wamefanya idea nyingi sana na wengine hadi wanakopi video za wenzao, wengine wanarudia vitu ili mradi tu kufanya video, lakini nikasema hiyo haiwezekani lazima wakati huu nifanye kitu ambacho kitamshangaza kila mtu," amesema.

"Vile vile ile ni kulisheshimisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania, nimewakumbuka nikasema nitafanya kitu gani hapa, ndio tukasema tufanye kama wanajeshi kwanza. Na Rudeboy kawakilisha jeshi la kwao katika njia ya usanii, ndio maana unaona pale nyuma kila mmoja ana bendera ya Taifa lake," Alikiba amekiambia kipindi cha Empire cha E FM Radio.

Kuhusu gharama za video hiyo, Alikiba amesema hawezi kuziweka wazi kwa sasa ila ni chini ya dola32,000 sawa na Sh74.2 milioni alizotumia kutengeneza video ya wimbo wake ‘Aje’.

Advertisement

"Kwangu video ya gharama kubwa ni Aje, nilitumia dola 32,000 pale Cape Town Afrika Kusini, hii (Salute) siwezi kusema lakini haijafikia huko, inaweza kwa video yangu ya tatu kwa kutumia gharama kubwa. Unaweza kufanya kitu kizuri lakini kwa bei rahisi na kikatoka kile kinachotarajiwa, video inakuwa ghali kutokana na aina ya maudhui unayotaka yawepo ndani yake" amesema Alikiba.

Katika hatua nyingine Alikiba amesema albamu yake ya tatu itatoka mwezi huu, kwani ilitakiwa kutoka Juni ila ikashindikana kwa sababu ilikuwa haijakamilika   upande mastering. Hadi sasa mwimbaji huyo wa Kings Music kashaachia albamu mbili ambazo ni ‘Ali K 4Real’ na ‘Cinderella’.


Advertisement