Basata yatengua maamuzi ya kumuengua Miss Tanzania kwenda Miss World

Thursday July 15 2021
misstanzanianyinginepic

Rose Manfere

By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limesema halijaridhia kuenguliwa kwa Miss Tanzania 2020/2021 Rosey Manfere, kushiriki mashindano ya Miss World yanayotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu Peutro Rico.
Hayo yamesewa leo Alhamisi Julai 15, 2021 na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Matiko Mniko katika mahojiano na Mwananchi Digital, iliyotaka kujua yaliyoafikiwa katika kikao kati ya baraza hilo na Rosey.
Kikao hicho awali ilikuwa kiwakutanishe Rosey, Basata na Kamati ya Miss Tanzania lakini ilishindikana baada ya wajumbe wa kamati kushindwa kufika kwa kile walichoeleza kuwa wamebanwa na majukumu mengine.
Hata hivyo Mniko amesema hilo halijawazuiya Basata kuja na uamuzi hayo ukizingatia kuwa ni kikao cha pili kufanyika baada ya cha kwanza kilichofanyika Mei 31 kushindwa kumalizika baada ya wajumbe kutofatiana.
"Moja ya maazimio tuliofikia baada ya kikao ni kwamba Baraza halijaridhia na halijakubaliana na maamuzi ya kumuengua Miss Tanzania 2020/2021 kwenye ushiriki wa shindnao la Dunia Miss World 2021 mpaka pale kamati ya Miss Tanzania itakapotoa sababu za msingi na kuzithibitisha.

"Kwa maelezo haya na kwa kuzingatia unyeti wa jambo hili, na kwa kuwa maandalizi ya mshiriki yanatakiwa kuendelea, Baraza linaelekeza yafuatayo;

"Kampuni ya “The Look” ambao ndio waandaji wa mashindano hayo, kuwasilisha jina la Miss Tanzania 2020/2021 Rosey Manfere, katika shindano la urembo la Dunia, 2021," amesema Mniko.

Maagizo mengine yaliyotolewa ni The Look kupeleka jina la Mkurugenzi mwingine badala ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Basila Mwanukuzi ambaye kwa sasa ana majukumu ya kiserikali yanayopelekea kutompata mara kwa mara pale wanapomuhitaji.

Basilla kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, nafasi aliyoanza kuitumikia tangu Juni 2021.
Wametakiwa kuwasilisha majina ya Wajumbe wa kamati ya Miss Tanzania na kuainisha nafasi zao kila mmoja.

Advertisement